Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kongwa imemhukumu kwenda jela miaka sita Ofisa Tabibu wa wilaya hiyo, Martine Ndahani kwa tuhuma za kumshawishi mwananchi ampe rushwa ya Sh 100, 000 ili mgonjwa wake awekewe damu.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kisasila Malangwa baada ya kuridhishwa na mashahidi tisa waliojitokeza kutoa ushahidi.
Upande wa mtuhumiwa ulikuwa na mashahidi watatu waliojitokeza kutoa ushahidi ambao haukuiridhisha mahakama.
Baada ya kusikikiza ushahidi wa pande zote, Hakimu Malangwa alimhukunu kwenda jela miaka sita au kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kila kosa alilosomewa.
Kesi hiyo ilikuwa chini ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma, Moshi Kaaya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema baada ya kufanya uchunguzi walimkamata mtuhumiwa huyo ambaye ni tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na kumfungulia mashtaka ambayo hukumu imetolewa.
Kibwengo alisema wananchi wanapaswa kushirikiana na Takukuru kutoa taarifa pale wanapoona kuna viashiria vya rushwa.
Wakati huo huo, Mahakama ya Wilaya ya Kondoa imemhukumu kwenda jela miaka minne, Jeremia Magawa aliyekuwa msimamizi wa miradi ya Kampuni ya FM Engineering iliyokuwa inasambaza umeme wa REA katika Kijiji cha Kiteo wilayani Kondoa.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mateso Masao baada ya kusikikiza ushahidi wa pande zote.
Mahakama ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alichukua jumla ya Sh 120, 000 kwa wananchi wawili ili awawekee nguzo za umeme karibu na nyumba.
Hata hivyo hakufanikiwa baada ya kunaswa na mtego wa Takukuru na kufikishwa mahakamani.
Kesi hiyo ilikuwa chini ya mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Haule.