Berlin, Ujerumani
Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz amechaguliwa na chama chake cha Social Democrats, SPD kugombea ukansela huku akiapa kuongeza kima cha chini cha mishahara iwapo watashinda uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba.
Waziri huyo wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz ameapa kuongeza kima cha chini cha mishahara baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba, akiwa na matumaina ya kupata uungawaji mkono wa karibu watu milioni 10 wanaolipwa kima cha chini, kukisaidia chama chake cha Social Democrats, SPD kutoendelea kupata matokeo mabovu.
Scholz ametoa ahadi hiyo kwa wajumbe wa chama hicho cha SPD waliompigia kura kugombea nafasi ya ukansela kutoka chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa shoto cha SPD. Meya huyo wa zamani wa Hamburg ameidhinishwa kwa asilimia 96.2 ya kura karibu 600 za wajumbe wa SPD, katika uchaguzi uliofanyika kwa njia ya mtandao mjini Berlin jana Jumapili.
Alisema “Kila kazi ina hadhi yake, kila kazi inastahili kuheshimiwa. Na hii ndio hasa inaakisi kiwango cha chini cha mshahara. Kisheria kiwango cha cha chini cha mshahara ni angalau € 12 kwa saa, kimepitwa na wakati.”
Uchunguzi wa maoni katika siku za karibuni umeonyesha chama chake kimekuwa nyuma ya vyama vya watetezi wa Mazingira ama Greens na vyama vya kihafidhina vya kansela Angela Merkel, lakini pia kikitabiriwa kushindwa vibaya kwenye uchaguzi.
Chama cha SPD kilijiunga bila ya kusita na muungano wa serikali ya vyama vya kihadhidhina ya kansela Merkel baada ya uchaguzi wa mwaka 2017, licha ya upinzani mkali kutoka kwa wanachama wake waliokuwa na hofu kwamba muungano huo wa mara ya tatu na Merkel huenda ukaathiti msimamo wa chama hicho juu ya wafanyakazi.