Na MWANDISHI WETU – ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameipongeza Serikali ya Cuba kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya.
Dk. Shein alisema kuna haja ya kuendelea na hatua hiyo kwa sekta nyingine ili kuzidisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na Balozi mpya wa Cuba nchini, Lucas Domingo Hernandez Polledo, Ikulu mjini Unguja, Dk. Shein alieleza kuwa Cuba ni nchi ya mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimweleza balozi huyo kuwa Cuba ina historia kubwa katika juhudi za kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo, hasa sekta ya afya kwani tokea mwaka 1966 nchi hiyo imekuwa ikipeka madaktari wake kwa awamu kwenda kufanya kazi Zanzibar.
Aidha alieleza kuwa mbali ya madaktari hao kutoa huduma ya afya kwa jamii, Cuba imekuza uhusiano wake kwa SMZ kwa kuanzisha chuo cha udaktari ambacho tayari kimetoa madaktari wazalendo ambao hivi sasa wanatoa huduma za afya hapa nchini.
Dk. Shein alisema: “Madaktari hao kutoka Cuba wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa huduma ya afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba usiku na mchana kwa kushirikiana na madaktari wazalendo.
“Zanzibar ina mengi ya kujifunza katika sekta ya utalii kutoka Cuba, kutokana na nchi hiyo kujiimarisha kwenye sekta hiyo na kupata mafanikio makubwa sambamba na kuendeleza vyanzo vyake vya utalii, likiwamo eneo maarufu la ukanda wa kitalii la ‘Varadero’.”
Naye Balozi Polledo alimweleza Dk. Shein kuwa Cuba inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuudumisha.
Balozi huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Cuba iko tayari kuendeleza uhusiano huo kwa kuimarisha sekta nyingine za maendeleo ikiwamo utalii, elimu na nyenginezo.