25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta amgeuka Dk. Mwakyembe

sittaSHABANI MATUTU NA ELIAS MSUYA, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Madeni Kipande, kwa tuhuma za utendaji mbovu, uliosababisha malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali.
Sitta amechukua uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo ambao umefikiwa baada ya kufanyika kwa kikao cha dharura cha Bodi ya Mamlaka ya Bandari kilichofanyika hivi karibuni.
Hatua hiyo ya Sitta imekwenda kinyume na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa akimwona Kipande ni mtendaji aliye makini.
Sitta alisema tangu kuingia kwa Kipande, kumekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwamo kutokuwapo uwazi katika utoaji wa zabuni zinazotangazwa na mamlaka hiyo.
Alisema kumekuwa na malalamiko kuhusu utoaji wa zabuni ambazo zimekuwa zikitolewa katika mazingira ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wadau mbalimbali, kwamba hazitolewi kwa uwazi, huku kukiwa na ubababaishaji kwa kamati za zabuni kubadilika mara kwa mara.
“Jamani bandari ni kituo muhimu kwa uchumi wa nchi wala haina haja ya kuelezea kwa kirefu, Takwimu zinaonyesha asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato hutokana na mfumo wa forodha, kati ya makusanyo hayo asilimia 87 yanakusanywa katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema.
Alisema pamoja na Waziri Mwakyembe kuyashughulikia malalamiko hayo, lakini bado bodi ya zabuni inapokuwa imetoa uamuzi kumekuwa na ucheleweshwaji wa kutoa barua ya kuwaruhusu wahusika kuanza kazi hali iliyokuwa ikizua taswira mbaya kwa Serikali na nchi kwa ujumla.
“Kwa vile mhusika mkuu ni Kaimu Mkurugezi Mtendaji, hivyo basi naamua kumsimamisha kazi hadi hapo tume niliyoiteua itakapokamilisha kazi ndani ya wiki mbili kuhusu malalamiko hayo,” alisema.
Sitta amemteua Meneja wa Bandari, Awadh Massawe, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wakati uchunguzi unapoendelea dhidi ya Kipande.
Pia ametangaza tume ya watu watano ambayo itafanya uchunguzi kwa wiki mbili kuhusu Kipande, ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa ya Kodi, Augusta Bubeshi.
Wajumbe wengine ni Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk. Ramadhan Mringa, mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi, Deogratias Kasinda pamoja na Samson Luhigo, Happines Semkoro na Flavian Kinunda ambao wote ni wastaafu kutoka idara mbalimbali za Bandari.
Sitta alisema sababu ya kuchukua wastaafu imechangiwa na ukweli kwamba hawana mpango wa kutaka cheo na watatenda kazi yao kwa kuzingatia haki.

KIPANDE AZUNGUMZA
Kwa upande wake, Mhandisi Kipande alipotakiwa kuzungumzia uamuzi huo uliochukuliwa na Waziri Sitta, alisema alifanya kazi kwa juhudi kadiri alivyoweza na Watanzania wataamua kuhusu hilo.
“Nimefanya kile ambacho kazi imetaka nifanye na naamini Watanzania wataamua katika utendaji wangu, hadi sasa bado mimi sijaona kosa nililofanya,” alisema.
Kipande alipata nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Ephrahim Mgawe pamoja na wasaidizi wake wawili ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za wizi.
Kutokana na kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo, Dk. Mwakyembe alimteua Mhandisi Kipande kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA.

MAKOSA YA KIPANDE
Taarifa ya ndani ya Waziri Sitta imeeleza makosa ya Kipande ikisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ipo katika kipindi cha misukusuko mikubwa ya kiutawala jambo linaloashiria hatari ya anguko kubwa la uchumi wa nchi yetu.
“Hatari hii itagusa kwa kiasi kikubwa nchi jirani ambazo tegemeo lake ni bandari za Mamlaka. Nchi hizi hupitisha wastani wa asilimia 30 ya jumla ya shehena yote inayohudumiwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam,”imesema taarifa ya Waziri Sitta na kuongeza:
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya makusanyo yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatokana na Kodi ya Ushuru wa Forodha (Customs and Excise Duty). Kati ya makusanyo hayo asilimia 87 yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Hii inaonyesha kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa katika makusanyo ya mapato ya taifa.”
Katika taarifa hiyo, Sitta amesema tangu ameingia wizarani hapo, amekuta matatizo makubwa ya kiutendaji yanayomhusisha Mtendaji Mkuu Kipande moja kwa moja ikiwa pamoja na uhusiano mbaya kati yake na wadau na wateja wa mamlaka, kukiuka kwa makusudi kwa taratibu za manunuzi na mahusiano mabaya kati yake na wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla wake.
Kuhusu uhusiano mbaya na wadau na wateja wa mamlaka, Sitta alidai tuhuma hizo zimeendelea kujenga taswira mbaya ya taasisi hiyo ambayo inafanya shughuli za kibiashara.
“Kwa ujumla vitendo hivi vina madhara makubwa na vikiendelea kuachwa vitaathiri biashara ya bandari ambayo kwa sasa inakabiliwa na ushindani mkubwa. “Nimepewa taarifa na mdau anayemiliki bandari kavu (ICD) hapa Dar es Salaam aliyefika ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka tarehe 05/02/2015. Katika mazungumzo na Mtendaji Mkuu alitolewa maneno makali na vitisho vingi na hatimaye akaambiwa kuwa ‘siogopi mtu yeyote katika Serikali hii, nenda popote sitasaini contract yako na nimeambiwa unataka kwenda mbele basi tutakutana huko’. Tuhuma hii kama ni ya kweli ni aibu kwa taifa,” alisema Sitta.
Aliongeza kuwa amekuta taarifa ya mtendaji huyo ya kumfukuza Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanga Cement aliyekwenda ofisini kwake kufuatilia maombi yao ya kupewa unafuu wa gharama katika bandari ya Tanga.
“Tanga Cement ndio watumiaji wakubwa wa bandari ya Tanga na miaka yote wamekuwa wanapewa punguzo la gharama kutokana na kuisaidia bandari ya Tanga ambapo hukodisha matishari (Barges) kutoka Mombasa ili kusaidia shughuli za kupakua meli zinazoleta shahena yao ya makaa ya mawe kupitia bandari hiyo,”alisema.
Alisema pia amekuta taarifa kuwa mwezi Januari mwaka huu aliwafokea na kuwafukuza wateja waliokuwa wamekuja kumwona kwa ajili ya mizigo yao iliyokaa muda mrefu bandarini.
Sitta alisema kuwa wateja hao wa Kampuni ya KRB Freight Ltd waliondoka kwa masikitiko makubwa.
Kwa upande mwingine, Sitta amezungumzia kukiuka kwa makusudi kwa taratibu za ununuzi.
Alisema mtendaji huyo alisitisha mchakato wa zabuni ya ujenzi wa gati Na. 4 katika bandari ya Mtwara.
“Usitishaji huo ameufanya baada ya kupata maelekezo ya wizara ya kuharakisha mchakato huo,”alisema Sitta na kuongeza:
“Mtendaji Mkuu amekuwa na kawaida ya kupinga mapendekezo ya Kitengo cha Ununuzi (Procurement Management Unit) kwa kuondoa baadhi ya majina yanayokuwa yamependekezwa katika timu ya wachambuzi wa zabuni (Evaluation Team) na kuweka majina anayotaka yeye kwa sababu anazozijua mwenyewe.”
Alisema amepata taarifa pia kwamba Mtendaji huyo Mkuu aliingilia mchakato wa zabuni ya mradi wa “Integrated Security System” kwa kuiondoa kampuni ambayo ilikuwa imeshinda zabuni hiyo kitendo ambacho kilifanya Benki ya Dunia kusitisha msaada kwenye mradi huo.
“Nimetaarifiwa pia kuwa sasa mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za mamlaka na unatekelezwa na kampuni iliyokuwa imekataliwa na Benki ya Dunia,” alisema Sitta.
Aliongeza kuwa mtendaji huyo alipotembelea Ubelgiji bila utaratibu, aliingia mkataba wa mradi mpya wa ‘Electronic Cargo Tracking Note’.
Alisema lengo la mradi huo ni kufuatilia na kupata taarifa za shehena yote inayoagizwa toka nje ya nchi na kusafirishwa kwa njia ya meli kupitia bandari za mamlaka.
“Kwa makusudi hakukuwa na ushirikishwaji wowote wa menejimenti wala wadau wa bandari na pia taratibu za zabuni hazikufuatwa.
“Mradi huu umekuwa na upinzani mkubwa toka kwa SUMATRA na wadau wa bandari kwa kuwa utazifanya bandari zetu kuwa ghali ikilinganishwa na bandari shindani.
“Hii inatokana na ukweli kuwa kila mwagizaji wa bidhaa angetakiwa kuilipa kampuni hiyo ya Kibelgiji wastani wa dola za Kimarekani 150 hadi 250 kwa kontena la futi ishirini,” alisema.
Alisema kama mradi huo utatekelezwa, wateja wengi wataikimbia bandari ya Dar es Salaam kutokana na ongezeko la gharama kwani hakuna bandari yoyote shindani inayotumia mfumo huo kwa sasa.
Kuhusu uhusiano mbaya kati yake na wafanyakazi wa mamlaka kwa ujumla wake, Sitta alidai kupata taarifa kwamba kauli na vitendo vya Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari vinakatisha tamaa katika kujenga ufanyakazi wa pamoja na morali kwa wafanyakazi wakiwamo wafanyakazi wake.
“Ninayo taarifa pia kuwa kwa maelekezo ya Mtendaji Mkuu kumekuwapo kwa uhamisho wa watendaji mbalimbali ambao hauna tija kwa shirika. Mara kadhaa baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakihamishwa kituo kimoja hadi kingine bila kuzingatia uwepo wa nafasi,” alisema katika taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles