NA SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM
TIMU sita za wanaume zilizoshika nafasi za juu kwenye Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), iliyomalizika hivi karibuni, zinatarajiwa kuchuana vikali kwenye mashindano ya ‘Super Cup’, Oktoba mwaka huu.
Mashindano hayo yenye lengo la kukuza vipaji pamoja na kutangaza mpira wa kikapu nchini, yanatarajiwa kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Chama cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Peter Mpangala, alizitaja timu hizo ni mabingwa watetezi Savio, JKT, Vijana, Oilers, Pazi pamoja na Magereza.
Mpangala alisema kwa sasa wanaendelea na maandalizi kuelekea mashindano hayo, ikiwamo mpangilio wa ratiba na tarehe rasmi ya ufunguzi wa michuano hiyo.
“Baada ya mshike mshike wa RBA kwa timu zote 26 kuvuna ilichopanda, sasa nguvu zote tunahamishia ‘Super Cup’ ambapo timu sita za juu ndizo zitakazochuana vikali kumpata bingwa.
“Nitoe wito kwa timu husika kujiandaa kikamilifu kwa mashambulizi dhidi ya kila mpinzani atakayekutana naye, pia milango ipo wazi kwa wadau kujitokeza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kikapu nchini,” alisema Mpangala.