Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Ikulu Dar es Salaam.
Kikao hicho cha dakika 45 kilifanyika jana huku wawili hao wakielezana yaliyo ndani ya mioyo yao.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa baada ya mazungumzo hayo, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.
Msigwa alisema kuwa Lowassa aliyataja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo na ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).
Mbali na hayo, alitaja pia ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mheshimiwa Rais (John Magufuli), tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo.
“Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo,” alisema Lowassa.
Alisema lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, elimu, kwani ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya.
“Hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mheshimiwa Rais (John Magufuli), you made my day,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake, Rais Magufuli, alimpongeza Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali na huku akimwelezea kuwa ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango wake katika nchi.
Alisema ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha urais, hakuwahi kumtukana.
“Mheshimiwa Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo (jana) nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Mheshimiwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri.
“Na mimi napenda kumpongeza Mheshimiwa Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.
“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Sh trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine,” alisema Rais Magufuli.
Mbowe amkana Lowassa
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Sauti ya Ujerumani (DW), Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kauli iliyotolewa na Lowassa si msimamo wa chama chake.
“Kama ni kweli hicho ndicho alichokizungumza huo si msimamo wa chama, sisi kama chama tunafanya maamuzi kupitia vikao na tunatoa maazimio ya pamoja baada ya kutafakari na kujadiliana kwa upana wake kuhusu hoja yenyewe.
“Katika siku za karibuni tumekuwa tuna malalamiko mengi dhidi ya Rais na Serikali yake, tumeona namna Rais anavyominya demorasia katika taifa na kunyima uhuru wa Bunge.
“Tume ya Uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama vinasaidia kuchafua chaguzi mbalimbali za marudio, tunaona namna zoezi haramu la kuwarubuni viongozi wa upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema.
Mbowe pia alielezea kushangazwa na kitendo cha Lowassa kudai kwamba Rais anatengeneza ajira hali ya kuwa hadi sasa bado kuna utata wa suala ajira kwa vijana.
“Mwenzetu Lowassa labda yeye ana takwimu zake tofauti na ambazo tunazijua kwa sababu amezungumzia kuongezeka kwa ajira, lakini hakusema kuongezeka kwa ajira ngapi japo amelinganisha kuwa ujenzi wa reli ya kati kunaweza kuongeza ajira.
“Tunaona kuna tatizo kubwa la ajira katika nchi na kuna ongezeko kubwa la vijana ambao hawana ajira, biashara zinafungwa, benki zinaelekea kufungwa na zote hizi ni ajira…..
Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTANZANIA.