Na MAREGESI PAUL – ALIYEKUWA SONGEA
WIKI iliyopita, tulieleza jinsi mwanafunzi Geofrey Ndungulu, alivyoanza masomo katika Shule ya Msingi Luhira na jinsi alivyokutana barabarani wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na mfanyabiashara wa madini, Ferdinand Masawe, ambaye ndiye aliyemsaidia kusoma na kufanikiwa kufika hapo alipo.
Katika makala haya, mfanyabiashara Masawe anaeleza ni kwanini aliamua kumsaidia Ndungulu na kumfikisha mahali alipo sasa.
Akizungumza na MTANZANIA hivi majuzi, mjini Songea, Masawe anasema hadi sasa hajui ni kwanini alikuwa na moyo wa kumsomesha kijana huyo baada ya kukutana naye barabarani ingawa amekuwa akiwasaidia watu mbalimbali wenye shida tofauti tofauti.
“Katika dunia hii, kila jambo linapangwa na Mungu kwa sababu hadi leo ukiniuliza ilikuwa kuwaje nikaamua kumsimamisha huyo kijana barabarani na kumuuliza historia ya maisha yake, naweza nisikupe majibu ya kuridhisha kwa sababu nilijikuta nikifanya hivyo.
“Nakumbuka siku niliyoonana na huyo kijana kwa mara ya kwanza, nilikuwa Mbinga
ziliko shughuli zangu za biashara ya madini na nakumbuka nilikuwa nikitembea barabarani.
“Kabla ya kumsemesha kitu, nilimuona akiendesha tairi la baiskeli akiwa na wenzake ambao sikumbuki idadi yao, lakini kati yao yeye ndiye alikuwa mkubwa kuliko wote.
“Nilipomuona tu, moyo wangu ulishtuka kidogo, nikajiuliza ni kwanini huyu mtoto ana umri wa kwenda shule, lakini anaonekana hasomi.
“Kwa hiyo, nilichokifanya nilimsimamisha hapo hapo barabarani, nikamsalimia, kisha nikamuuliza kwanini hasomi wakati umri wake ni wa kwenda shule.
“Kwa bahati nzuri hakunificha, aliniambia ana matatizo ya macho na hapo tulipokuwa tumesimama, alikuwa hanioni vizuri.
“Akaniambia pia kwamba, anapenda sana shule, lakini hasomi kwa sababu ya hayo matatizo ya macho na mama yake ni maskini hana uwezo wa kumpeleka hospitali akatibiwe na kumsomesha kwa sababu baba yake alishafariki.
“Nilipokuwa nikiongea naye, kuna mambo nilikuwa najifunza kutoka kwake na baadaye nikamuuliza kwa hiyo nikikupeleka hospitali ukatibiwe na kupona, utakubali kuanza shule?
“Hapo alinijibu kwamba yuko tayari na anapenda kusoma ila anashindwa kwenda shule kutokana na umaskini wa familia yake.
“Kwa hiyo, nilichokifanya ni kwenda nyumbani kwao, nikaonana na mama yake, nikamweleza nia yangu ya kumtibu mtoto wake na kumsomesha kadiri nitakavyoweza, japokuwa alikuwa hanifahamu kabisa.
“Kwa bahati nzuri, yule mama alinikubalia, kwahiyo, tulipanga siku ya kwenda hospitali kwa ajili ya kuanza matibabu ya mtoto wake,” anasimulia Masawe.
Kwa mujibu wa Masawe, baada ya kukubaliana na mama yake Ndungulu, walipanga siku ambapo aliwachukua na kumpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, ambako aliamini ndiko kuna madaktari bingwa wa macho.
Anasema baada ya kufika hospitalini hapo, baadhi ya madaktari na wauguzi hawakumwelewa alikuwa na lengo gani kumtibu Ndungulu baada ya kugundua hakuwa mtoto wake na hana undugu naye wa aina yoyoye.
“Mwanzoni madaktari na baadhi ya wauguzi walipojua mtoto huyo hakuwa mwanangu na hakuwa ndugu yangu, hawakunielewa nina lengo gani la kumsaidia matibabu.
“Pamoja na hali hiyo sikukata tama, mwishowe nilionana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho, aliyekuwa anaitwa Dk. Kahabuka ambaye alimpima kitaalam baada ya kugundua tatizo alimpa dawa na kumwandikia miwani ambapo gharama zote nililipa mimi.
“Baada ya hatua hiyo, nikaanza kutafakari ni shule gani ntampeleka ili aanze masomo kwa sababu nilikuwa tayari nimeshaamua kumsaidia.
“Niliwaulizia watu mbalimbali kuhusu masuala ya shule, baadaye mtu mmoja akaniambia shule inayomfaa Ndungulu ni Luhira Shule ya Msingi iliyoko Mshangano, Manispaa ya Songea kwa sababu pale wanafundisha watoto wenye mahitaji maalum wakiwamo wasioona kabisa na wenye uoni hafifu kama yeye.
“Nilifanya taratibu zote zilizokuwa zikitakiwa kuingia shuleni hapo nikafanikiwa.
“Jambo la kufurahisha ni kwamba, alipoanza darasa la kwanza, alionyesha maajabu darasani kwa sababu alionekana ana uwezo mkubwa na hapo
akaanza kurushwa madarasa hadi alipohitimu elimu ya msingi baada ya miaka mitano badala ya miaka saba kama ilivyo kawaida.
“Alipofaulu kuanza masomo ya kidato cha kwanza pale Songea Boys, mimi, mke wangu na watoto wetu, tulifarijika kwa sababu tuliona sasa neema inaanza kuingia nyumbani kwetu kwa kumsaidia mtu anayehitaji msaada.
“Kwa kweli namshukuru Mungu kwa hatua hiyo niliyomfikisha mwanafunzi huyo kwa kumsomesha kwa asilimia 100 kwa sababu naamini Mungu ndiye aliyenikutanisha naye barabarani.
“Kwa kuwa sasa anaonekana kufika pazuri, naiomba Serikali impe mkopo kwa asilimia 100 kwani uwezo wangu wa kuendelea kumlipia ada ya
chuo kikuu kwa asilimia 100 sina kwani uchumi wangu kwa sasa umeyumba na majukumu ninayo mengi.
“Pamoja na hayo, bado Ndungulu namchukulia kama mwanangu na mdogo wangu pia kwa sababu nimemtoa mbali na naamini Mungu ana makusudi yake kuniunganisha kupitia mazingira ya kutatanisha,” anasimulia Masawe.
Wakati huo huo, Masawe anasema pamoja na kwamba amekuwa akitumia muda mwingi kuwa karibu na Ndungulu, jambo la ajabu ni kwamba mwanafunzi huyo yuko karibu na mkewe pamoja na watoto wake watatu.
“Pamoja na kwamba mimi ndiye niliyemleta nyumbani, mapenzi yake makubwa yako kwa mke wangu pamoja na watoto wangu.
“Yaani, anawapenda sana wanangu na anamheshimu mke wangu kiasi kwamba baadhi ya mambo haniambii bali anamwambia mke wangu na hata akiwa na akiba ya fedha, anampa mke wangu amtunzie,” anasema Masawe.
MAMA YAKE NDUNGULU ATOA NENO
Wakati Masawe akisema hayo, mama mzazi wa Ndungulu aliyejitambulisha kwa jina la Veronica Nditi (63), anasema alichokifanya Masawe hakuwahi kukifikiria katika maisha yake.
Nditi ambaye alizungumza na MTANZANIA akiwa nchini Msumbuji katika Mtaa wa Seli, Wilaya ya Mitengula, mkoani Nyasa, anasema kama asingekuwa Masawe, mtoto wake huyo angekuwa na maisha ya shida kwa kuwa hakukuwa na mtu wa kumsaidia.
“Mimi nina watoto wanane na hadi sasa hakuna aliyesoma kama huyo Ndungulu ambaye ni mtoto wangu wa saba kuzaliwa.
“Kutokana na matatizo yake ya macho aliyonayo, nilikuwa nimeshakata tamaa ya kumsomesha kwa sababu mimi ni masikini na ni mjane, mume wangu niliyeishi naye miaka 30, alifariki mwaka 2003.
“Huku Msumbuji ninakoishi kwa sasa kuna watoto wangu watatu walihamia huku, kwa hiyo, nimekuja kwa muda kuwasalimia na baadaye nitarudi nyumbani kwangu Mbinga, Mkoa wa Ruvuma.
“Kuhusu Ndungulu, ni kwamba kabla hajasaidiwa na Masawe, ndugu zangu na wanangu wengine walikuwa wamemkataa wakawa wananiambia hawawezi kuishi na mtu asiyeona kwa sababu atawasumbua katika maisha.
“Kwa hiyo, alipojitokeza Masawe na kutaka kumsaidia, mwanzoni nilishtuka, lakini aliponieleza nia yake kwa undani zaidi na akasema huko hospitalini Songea na mimi nitamsindikiza siku atakapokwenda kutibiwa, nikakubali japo kwa shingo upande.
“Yaani, hata tulipokuwa njiani kuelekea hospitalini Songea, bado nilikuwa na mashaka na nikawa najiuliza huyu Masawe ni mtu wa aina gani anayejitolea kumsaidia mtu aliyekutana naye barabarani?
“Lakini, baada ya kufika hospitalini na mwanangu kuanza kutibiwa, moyo wangu uliumia sana kwa sababu sijui nitamlipa nini Masawe na jambo la kushangaza zaidi, ni kwamba Masawe ananichukulia kama mama yake kwani mara nyingi nimekuwa nikienda nyumbani kwake Songea mjini kumsalimia.
“Kwa hiyo, ninachoweza kusema ni kwamba, Masawe ni mwanangu pia kutokana na jinsi alivyomsaidia mwanangu huyo, kwani bila yeye, mwanangu asingefika hapo alipo,” anasema Nditi.
Kama alivyosema Masawe, kwamba anaiomba Serikali imsaidie kumsomesha Ndungulu, Nditi naye anaiomba Serikali ifanye hivyo kwa kuwa yeye binafsi hana uwezo wa kumsomesha mtoto wake huyo kwa kuwa Masawe kwa sasa anakabiliwa na majukumu mengi.
Makala haya yataendelea wiki ijayo ambapo walimu waliomfundisha Ndungulu akiwa shule ya msingi na sekondari, wataeleza maajabu aliyokuwa akiyafanya akiwa darasani.