*Yanga nayo hakuna kuchelewa, yaibukia kibabe Mtibwa Sugar
THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wamewasili salama jijini Tanga, tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho Uwanja wa Mkwakwani.
Mara baada ya kuwasili jijini humo jana wakitokea Dar es Salaam, msafara wa kikosi cha Simba ulipokewa na mamia ya mashabiki wa timu hiyo waliokuwa na shauku ya kuwaona mastaa hao.
Simba ilitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kuondolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kuchapwa mabao 4-1, katika mchezo wa marudiano uliochezwa Jumamosi iliyopita, Uwanja wa Mazembe, jijini Lubumbashi.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Simba ilishindwa kutamba baada ya kulazimishwa suluhu na Wakongomani hao.
Mafanikio hayo ya Simba, yameiwezesha Tanzania kupata fursa ya kuingiza timu nne katika michuano ijayo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, ambao kila moja itapewa nafasi mbili kulingana na taratibu za Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Akizungumza na MTANZANIA jana, kocha wa viungo wa Simba, Adel Zrane, alisema:
“Tumefika salama Tanga, tutapumzika kisha jioni tutafanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kujiweka fiti,” alisema Zrane.
Simba katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Wekundu hao wa Msimbazi, wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa na pointi 57, baada ya kushuka dimbani mara 22, wakishinda michezo 18, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.
Nao vinara wa Ligi Kuu, Yanga, tayari wamekanyaga ardhi ya Morogoro, wakisubiri kuivaa Mtibwa Sugar kesho, Uwanja wa Jamhuri.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 27, kama ilivyo kwa wapizani wao Simba, nao walisafiri kwenda Morogoro jana wakiwa na kikosi cha wachezaji 20.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alisema kikosi chao kilifika salama Mji kasoro bahari kama baadhi ya watu wanavyopenda kuuita, ambapo jioni kilifanya mazoezi mepesi.
“Wachezaji 20 ndio waliokwenda Morogoro, wengine waliobaki ni majeruhi na wengine wanatumikia adhabu ya kadi, lakini hata hivyo waliokwenda wapo vizuri na kila mmoja ana ari,” alisema.
Yanga inashika usukani wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 74, ilizozipata kupitia michezo 31, ikishinda 23, sare tano na kupoteza mitatu.