WINFRIDA NGONYANI NA ADAM MKWEPU-DAR
BAADA ya kutoswa katika usajili wa mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo, uongozi wa klabu ya Simba umemleta straika mwingine raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Masoud Masanga, ili kuziba pengo hilo.
Mshambuliaji huyo aliyetua nchini juzi akiwa na mwenzake, wamekuja kwa majaribio wakitokea katika klabu ya St Eloi Lupopo FC ya Lubumbashi, tayari kujiunga na kikosi cha Simba kilichopo kambini mkoani Morogoro.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Kahemele, alisema baada ya Mavugo kutimkia klabu ya Tours FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa, uongozi umeona kuna umuhimu wa kutafuta washambuliaji wenye uwezo unaofanana na nyota huyo.
“Mavugo ni straika mzuri mwenye kiwango cha kimataifa, lakini ni vigumu kumzuia asifanye anachopenda wakati tayari alikuwa na nafasi ya kwenda kujaribu bahati ya kucheza soka barani Ulaya,” alisema Kahemele.
Aidha, Kahemele aliongeza kuwa wachezaji hao watafanya majaribio chini ya Kocha Mkuu wa Simba Mcameroon, Joseph Omog ambaye ataweza kuwaidhinisha kujiunga na timu kama ataridhishwa na viwango vyao.
“Kocha Omog atakuwa na jukumu la kuhakikisha wachezaji hawa wanafanyiwa majaribio na kuchujwa kutokana na vigezo ambavyo vinahitajika ili kutengeneza kikosi bora na imara kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao,” alisema Kahemele.
Mavugo alitimkia nchini Ufaransa na kuachana na klabu ya Simba ambayo ilikuwa ikimuwinda tangu msimu uliopita, huku ikidaiwa kumlipa straika huyo sehemu ya fedha ya usajili wake wakati wakisubiri amalize mkataba wa kuichezea Vital’O kwa mwaka mmoja.