32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAINYOOSHA YANGA

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imeifunga Yanga mabao 2-1 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Mathew Akrama kutoka Mwanza, Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tatu lililofungwa na Simon Msuva kwa penalti baada ya beki Novalty Lufunga, kumwangusha mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, katika eneo la hatari.

Kuingia kwa bao hilo kuliwachanganya wachezaji wa timu ya Simba, kwani katika dakika chache tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Javier Bukungu, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Chirwa.

Pamoja na kutolewa kwa Bukungu, Simba walikuja juu na kuliandama lango la Yanga na katika dakika ya 13, Laudit Mavugo, alikosa bao baada ya kuchelewa kumalizia pasi ya Juma Luizio.

Katika kujiimarisha Simba walifanya mabadiliko katika dakika ya 26 kwa kumtoa Luizio na kuingia Said Ndemla.

Simba walipata nafasi nyingi za kufunga lakini walipoteza kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini.

Katika dakika ya 43, Thaban Kamusoko, alitolewa nje baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Said Makapu, hata hivyo Yanga walikwenda mapumziko wakiwa mbele wanaongoza kwa bao 1-0.

Katika mchezo huo uliokuwa na upinzani wa aina yake, ulihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu, aliyejiunga na chama hicho akitokea CCM.

Kipindi cha pili kilianza huku Simba wakionekana kurudi na ari mpya, kwani katika dakika 46, mshambuliaji Ibrahim Ajib alikosa bao baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba.

Simba walifanya mabadiliko katika dakika ya 51 kwa kumtoa Novalty Lufunga na kuingia kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya.

Katika kuimarisha kiungo, Simba walifanya tena mabadiliko katika dakika ya 57 kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha mkuu, Joseph Omog, yaliinufaisha timu hiyo baada ya Mavugo kuisawazishia bao timu hiyo katika dakika ya 67 baada ya kuwahadaa mabeki wa Simba, akipokea pasi kutoka kwa Kichuya. 

Kuingia kwa bao hilo kuliwavuruga Yanga kwani katika dakika ya 70 walifanya mabadiliko kwa kumtoa Amissi Tambwe na kuingia Deus Kaseke.

Mabadiliko mengine kwa Yanga yalifanywa katika dakika ya 78 kwa kumtoa Justine Zulu na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi.

Aliyepeleka kilio kwa mabingwa watetezi wa kombe hilo, alikuwa ni Kichuya aliyefunga bao la pili kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Yang,a Deogratius Munish ‘Dida’ katika dakika ya 80 baada ya kupokea pasi ya Jonas Mkude.

Hadi dakika 90 zinamalizika, Simba walichomoza na ushindi wa mabao 2-1.

Katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Kwa matokeo hayo Simba inazidi kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 54 na hivyo kujiweka vizuri katika kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, huku watani wao wakibaki nafasi ya pili wakiwa na pointi 49.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles