MOHAMED KASSARA na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM
NI baada ya miaka nane timu za Simba na TP Mazembe, zinakutana tena katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kukutana kwa timu hizo kumetokea, baada kupangwa kumenyana katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba itaanzia nyumbani katika mchezo wa mkondo wa kwanza, utakaochezwa Aprili 5, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kurudiana jijini Lubumbashi Aprili 12.
Wekundu hao wa Msimbazi walifuzu hatua hiyo, baada ya kufikisha pointi tisa na kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi D, wakati TP Mazembe ilimaliza kinara wa kundi C na pointi 10.
Mshindi wa jumla kati ya TP Mazembe na Simba, atakutana na mbabe kati ya Constatine ya Algeria na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Esperance ya Tunisia katika hatua ya nusu fainali.
Mara ya mwisho Simba kukutana na TP Mazembe ilikuwa mwaka 2011 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, Wekundu hao waliambulia kipigo cha mabao 3-1 Lubumbashi, kabla ya kuchapwa tena mabao 3-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hivyo kujikuta wakitolewa kwa jumla ya mabao 6-3.
Kwa wakati huo, TP Mazembe ilikuwa ikiundwa na wachezaji wakali kama Tresor Mputu, kipa Robert Kidiaba, Given Sunguluma, Stopilla Sunzu, Rainford Kalaba na Mihayo Kazembe.
Simba ya wakati huo, ilikuwa na kipa Juma Kaseja, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Jerry Santo, Patrick Ochan, Mussa Hassan ‘ Mgosi’, Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta.
Michezo hiyo miwili ndiyo iliyoanzisha safari ya Samatta katika anga za kimataifa, kwani alicheza kwa kiwango cha juu na kufunga bao moja katika mchezo wa pili Uwanja wa Taifa.
Baadaye TP Mazembe, ilimnunua Samatta pamoja na Ochan, baada ya kuvutiwa na uwezo wao.
SPOTIKIKI linakuchambulia vikosi vya timu hizo vitakavyoshuka dimbani kutoana jasho katika hatua ya robo fainali, baada ya kuacha kwa miaka nane, huku kila moja ikiwa na sura za wachezaji tofauti.
Pia maoni ya wachezaji wadhamani waliwahi kuichezea timu hiyo pindi ilipofanikiwa kufanya vema katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
SIMBA
Timu hiyo ilianzia hatua ya awali ya michuano hiyo kwa kuvaana na Mbabane Swallows ya Eswatini, katika mchezo wa kwanza nyumbani, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Wekundu hao wa Msimbazi waliendeleza rekodi zao nzuri nyumbani katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya michuano dhidi ya Nkana Red Devils na kushinda kwa mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi.
Katika hatua ya makundi Simba, ilikuwa miongoni mwa timu zilizonufaika na matumizi mazuri ya uwanja wa nyumbani kwa kuvuna pointi tisa zilizowapeleka robo fainali ya michuano hiyo.
Katika michezo hiyo, Simba ilianza kwa kuicharaza JS Saoura mabao 3-0, ikaichapa Al alhly bao 1-0, kabla ya kufunga hesabau kwa kuidungua AS Vita mabao 2-1.
Simba imefanikiwa kufikia hatua hiyo kutokana na matumizi mazuri ya uwanja wao wa nyumbani, ambako wameshinda mechi zao zote tano za kuanzia hatua ya awali hadi makundi.
Katika michezo hiyo, Simba inajivunia safu kali ya ushambuliaji ambayo imepachika mabao 12 katika michezo hiyo ya nyumbani.
Mshambuliaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Simba ni Meddie Kagere, aliyepachika mabao matatu katika hatua ya makundi.
Ukiachana na Kagere, yupo mshambuliaji John Bocco aliyefunga mabao mawili katika michuano ya kimataifa.
Kiungo Clotus Chama ni habari nyingine katika ufungaji, kwani amepachika mabao matano hadi sasa katika michuano ya kimataifa, akifunga mabao manne katika hatua ya awali na raundi ya kwanza, kabla ya kufunga bao moja kwenye hatua ya makundi lililoipelela Simba robo fainali.
Kuelekea mchezo huo, Simba itakuwa na mchezaji mmoja pekee aliyekuwa katika kikosi hicho wakati timu hizo zilipovaana mara ya mwisho.
Mchezaji huyo ni mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi ambaye pia alifunga moja ya mabao ya Simba katika michezo hiyo miwili.
Mbali na Okwi, pia Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems anaifahamu vema TP Mazembe kwa kuwa tayari ameshakutana nao kwenye michezo ya ligi alipokuwa anainoa timu ya AC Leopards ya DRC.
Katika misimu miwili ambayo ameinoa timu hiyo, Aussems hajapoteza mchezo wowote dhidi Mazembe.
TP MAZEMBE
Mazembe imetwaa taji hilo mara tano na kushika nafasi ya pili, nyuma ya Al Alhly ya Misri ambayo ndiyo kinara baada ya kunyakua ubingwa huo mara nane.
TP Mazembe ilitwaa ubingwa huo mwaka 1967,1968,2009,2010 na 2015, ina kikosi cha wachezaji 34 ambacho wastani wa umri wa wachezaji hao ni miaka 26.
Timu hiyo ina wachezaji 12 wakigeni kutoka nje ya DRC, watatu wakitokea Zambia, Ivory Coast (watatu) , Mali na Ghana, kila moja wawili, wakati nchi za Uganda, Cameroon na Ubelgiji zikichangia mchezaji mmoja.
TP Mazembe ni tishio kwenye safu ya ushambuliaji, ambayo msimu huu wa Ligi Kuu ya DRC, imefunga mabao 54, kupitia michezo yake 23.
Wanashilikilia rekodi ya kuvuna ushindi mkubwa zaidi kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuitungua Club African ya Algeria mabao 8-0.
Kama hiyo haitoshi, ndiyo timu iliyoongoza kwa kufunga mabao mengi katika hatua ya makundi, ikipachika mabao 13.
Wachezaji hatari kwenye kikosi kicho ni Jackson Muleka, Kelvin Mondeko Zatu na Tresor Mputu ambao wote kwa pamoja wamefunga mabao tisa, kati ya 13 ya timu hiyo katika hatua ya makundi.
Mazembe wanao ukuta mgumu unaoongozwa na mlinda mlango wao raia wa Ivory Coast, Sylvain Gbohouo, ambao hadi sasa umeruhusu mabao 14, katika michezo 23 ya ligi na mabao manne kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa.
Hata hivyo, timu hiyo ina wachezaji wengi wenye umri unaozidi miaka 30, watano kati hao wanacheza eneo la ulinzi.
Wachezaji wanaozidi miaka 30 ni Gbohouo(30), Aime Bakula (34),Joel Kimwaki (32),Kilitcho Kasusula(36), Issama Mpeto (33),Rainaford Kalaba (32) na Mputu mwenye miaka 33.
Mazembe itakuja nchini ikiwa na wachezaji wake watatu, walikuwamo katika kikosi kilichoikabili Simba mwaka 2011.
Wachezaji hao ni Mputu aliyekuwa nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Rainford Kalaba na kocha wao, Mihayo Kazembe aliyekuwa akichezea nafasi ya kiungo kwa wakati huo.
Wachezaji wa zamani wa Simba
Fikiri Magosso anasema wachezaji wanastahili pongezi kwani kwa kiasi kikubwa wamepambana, haikuwa kazi nyepesi, wamefungwa mabao mengi kwenye kundi lao, ila wamepata matokeo mazuri nyumbani.
“Wameweza kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kusaka matokeo, ukweli halisi wanatakiwa kupambana kwani wanaijua vema TP Mazembe, sio timu ya kuizarau hata kidogo, tunaposema mapambano makali ndio sasa yanahitaji.
George Masatu hatua waliyofikia ni nzuri, kinachotakiwa ni kusaka matokeo mazuri,kila mmoja anatakiwa kuwa mwalimu wa mwingine, enzi zetulifanikiwa sababu ya kushirikiana yani wote tulikuwa kitu kimoja.
“Mfano mdogo ni kuwa tayari hawa wanakitu kizuri karibu yao, yani bado kukishika tu na hilo linawezekana wakiamua na kuonyesha juhudi,”anasema.
Wachezaji wanatakiwa kuonyesha ushirikiano, wapendane, wote wanatakiwa kuwa kitu kimoja, wapo kazini hivyo lazima wapiganie nchi na jina la klabu.
Malota Soma kitu kinachotakiwa ni maandalizi mazuri, wajipange huko mbele timu zimejipanga, kila mchezaji anatakiwa kufahamu anaenda kufanya nini uwanjani.
“Wachezaji wajue hatua waliyofikia ni ngumu zaidi ya walipotoka, huko mbele hakuna kuzembea kwani lazima mtakuta wapinzani wamejiandaa na kuwawekea mbinu za kuwashinda,”anasema
Anasema wachezaji wajue wanakoenda ni kugumu zaidi,sisi tulifanya vizuri kutokana na mikakati tuliyojiwekea, kuhakikisha tunapata mabao mengi nyumbani, hivyo hata ugenini ilikuwa raisi kwetu kuwabana wapinzani, lakini jambo la muhimu ni kusikiliza mafundisho ya mwalimu.W