26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, JKT Tanzania vita ya kihistoria

NA SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara, inaendelea leo kwa michezo mitatu kupigwa kwenye viwanjani tofauti hapa nchini.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba itajitupa katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma, kukabiliana na wenyeji wao JKT Tanzania, Bishara United itakuwa nyumbani Uwanja wa Karume mjini Musoma kuumana na Mtibwa Sugar, wakati ambao Azam FC itakuwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, kupepetana na Kagera Sugar.

Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gwambina, mchezo uliochezwa Septemba 26, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Katika msimamo wa ligi hiyo kabla ya michezo iliyopigwa jana, Simba ilikuwa katika nafasi ya pili, ikiwa na pointi 10, baada ya kushuka dimbani mara nne, ikishinda michezo mitatu na sare moja.

Kwa upande wake, JKT Tanzania kabla ya michezo iliyopigwa jana, ilikuwa kwenye nafasi ya 14 ikiwa na pointi nne, baada ya kushuka dimba ni mara nne, ikishinda mchezo mmoja, sare moja na kupoteza miwili.

Itawakabili Wekundu hao wa Msimbazi ikitoka kuchapwa bao 1-0 na Coastal Union, mchezo uliochezwa Septemba 28, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Timu hizo zilipokutana msimu uliopita wa ligi hiyo, Simba ilishinda mabao 3-0, lakini ziliporudiana JKT  Tanzania iliibuka mbabe kwa bao 1-0, michezo myote ikichezwa Uwanja wa Mkapa.


Kwa ujumla rekodi za michezo iliyozikutanisha timu hizo inaonyenyesha zinapokutana kunakuwa na ushindani mkubwa kiasi kwamba hakuna anayevuna pointi tatu kirahisi. 

Kuelekea mchezo huo, makocha wa timu hizo kila mmoja amejigamba kuibuka na ushindi ili kujiongezea pointi tatu nyingine kwenye akiba yao.

“Tunakwenda Dodoma tukiwa na  hari ya mchezo baada ya kushinda idadi kubwa ya mabao kwenye michezo yote miwili tuliyocheza  nyumbani.

Ni matumaini yangu tulichokifanya nyumbani ambacho ni kupata ushindi  kwenye michezo yote miwili tutaendelea nacho dhidi ya JKT Tanzania,”alisema Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbloeck.

Katika mchezo huo, Sven huenda akamwanzisha mshambuliaji Chrispine Mugalu, ambaye licha ya kuanzia benchi kwenye michezo iliyopita aliyopata nafasi alifanikiwa kufunga bao.

Kwa upande wake, Kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Bares alisema hawataki kurejea makosa ya mchezo wao uliopita hivyo wataingia uwanjani  na nguvu kubwa ya kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi.

“Tulipoteza mchezo dhidi ya Coastal  lakini pia tulipoteza mchezo Dodoma Jiji, hatutakuwa tayari  kuona Simba inachukua pointi tatu kwenye uwanja wetu wa nyumbani.

“Tutaingia uwanjani kupambana na wachezaji wangu wako fiti kwa ajili ya mchezo huo,”alisema.

Biashara itakayoumana na Mtibwa ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi saba, baada ya kushuka dimbani mara nne, ikishinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Mtibwa Sugar kwa upande wake ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi tano, ilizozipata baada ya kushuka dimbani mara nne, ikishinda mchezo mmoja, sare mbili na kuchapwa mara moja.

Azam itakayoikaribisha Kagera Sugar, inakamata uongozi wa ligi hiyo ikiwa na pointi 12, ilizozipata baada ya kushuka dimbani mara nne na kushinda michezo yote.

Kagera yenyewe imeshuka dimbani mara nne, ineshinda mchezo mmoja, sare moja na kuchapwa mara moja, hivyo kukamata nafasi ya 12. Msimamo huo ni kabla ya michezo ya jana.

Michezo iliyochezwa jana mchana na jioni, Mbeya City na Tanzania Prisons , zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu Uwanja wa Sokoine Mbeya, Gwambina ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0  dhidi ya  Ihefu, Mwadui ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles