Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shule ya Msingi Nuru Angavu iliyoko Mwanagati, Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam imefanya vizuri Matokeo ya Darasa la saba kwa mwaka 2023, Ki-mkoa imeshika nafasi ya nane kwa upande wa shule zenye idadi ya watahiniwa chini ya 40 kwa darasa.
Meneja wa shule hiyo ya mchepuo wa Kiingereza, Mary Kimaro amesema kuwa siri ya mafanikio ya shule yake ni ushirikiano baina ya wazazi, waalimu na mamlaka zinazosimamia elimu nchini.
“Bila ushirikiano huo tusingefikia hapa, utaona umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha jambo lolote lile,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuwa maeneo yanayoizunguka shule yao na jijini la Dar es Salaam kwa ujumla kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shuleni hapo ili wapate elimu bora.
Ameongeza kuwa shule yake imeongoza katika Kata yao ya Mzinga na kwamba wamejipanga kufanya vizuri zaidi siku zijazo.
Amesisitiza kuwa wamejipanga kukuza vipaji vya vijana iwe katika masomo au michezo kwa ujumla kwani vipaji katika Dunia ya sasa vinalipa.
“Pamoja na mambo mengine shule yetu inasomesha vijana 30 bure ambao wanatoka katika familia duni wenye uwezo wa kimasomo.
“Tunasaidia vijana hawa ili kuwawezesha kupata elimu bora hata kama hawana uwezo wa kiuchumi.
“Wito wangu kwa taasisi mbalimbali kushirikiana na taasisi yetu katika kuwasaidia vijana hawa,” amesema.