NA OSCAR ASSENGA
SHIRIKISHO la Vyuo vya Elimu ya Juu mkoani Tanga limeitaka serikali iwachukulie hatua kali watu waliotajwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya iwapo watabainika kutumia.
Limesema ni muhimu pia kuwabana wafanyabiashara wa dawa hizo kuweza kuumaliza mtandao huo.
Shirikisho hilo pia limeunga mkono juhudi zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda la kupambana na watumiaji wa dawa za kulevya mkoani humo.
Limewataka wakuu wa mikoa mengine kuunga mkono suala hilo.
Mwenyekiti wa Shirikisho hilo mkoani Tanga, Justus Gration alikuwa akizungumzia hatua ya Makonda kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.
Alisema suala la utumiaji wa dawa za kulevya haliwezi kumalizika iwapo watanzania hawatakuwa na ushirikiana wa dhati kwenye mapambano hayo kwa kuwafichua wahusika.
Gration alisema hatua hiyo itaiwezesha jamii kuepukana na tatizo hilo.
“Kimsingi naunga mkono jitihada za serikali kupambana na kutokomeza dawa za kulevya.
“Kwa moyo wa dhati kabisa nampongeza RC Makonda kwa juhudi anazozichukua lakini pia watanzania tuendelee kumpa ushirikiana kuendelea kufichua magenge makubwa yanayohusika.
“Lakini vita ya dawa za kuveya isiishie mkoani Dar es Salaam pekee bali yawe ni mapambano nchi nzima.
“Jambo hilo limeathiri vijana wengi na kama likifika mkoani Tanga mimi nitakuwa tayari kuunga mkono,” alisema
Aliwataka vijana shuleni kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa kuwafichua baadhi yao ambao wanajuhusisha na matumizi hayo.
“Nisisitize tu endapo wanaotajwa kutumia dawa aa kulevya au kuziingiza nchini wakikutwa na hatia nashauri serikali iwachukulie hatua kali na nzito ili kuutokomeza mtandao huo ambao ni hatari kwa maendeleo,“ alisema.