Malima Lubasha
SEKTA ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu kwa uchumi wa taifa kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa na kusaidia uhifadhi wa raslimali za misitu, wanyama na mandhari ya kihistoria inayotumika kama maeneo ya kujifunzia na yenye mchango katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Ili kuimarisha na kuifanya sekta ya utalii iwe endelevu, Serikali, taasisi binafsi na wadau wa utalii kila mmoja kwa nafasi yake wamekuwa wakiweka jitihada zao kujenga mazingira rafiki na sera wezeshi zinazochagiza maendeleo ya utalii nchini.
Yote yanayofanyika tunaamini yanalenga kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kufanikiwa zaidi ili watalii kutoka ndani na nje ya nchi wanaohitaji au wale wanaobahatika kutembelea vivutio na hifadhi kwenye eneo lolote nchini wasikumbane na vikwazo, ama taharuki ya aina yeyote badala yake wafurahie matembezi yao.
Tunatambua zipo sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza watalii wanaotembelea maeneo ya hifadhi zenye makusudio makuu mawili kwanza kabisa kulinda usalama wao na pili kuwaongoza watalii kukamilisha malengo yao pasipo kuvunja sheria za nchi ingawa miongoni mwake zimetajwa kuwepo baadhi ya sheria zenye mapungufu zinazoonekana kutowapa watalii uhuru wa kutosha.
Moja ya sheria ambayo imeendelea kulalamikiwa sana na watalii pamoja na wadau kwenye sekta hii ni ile inayojulikana kama ‘Single Entry’ inayomlazimisha mtalii anapoingia ndani ya hifadhi kulipia na kukaa ndani ya hifadhi hadi atakapomaliza shughuli zake na iwapo atatoka nje hata baada ya dakika mbili akirudi atatakiwa kulipia upya.
Sheria hiyo inatajwa kuchangia sana kurudisha nyuma maendeleo ya utalii kwa kuwa mtalii analazimika kukaa ndani ya hifadhi mpaka muda wake utakapofika mwisho hali ambayo inamkosesha uhuru wa kutembelea vivutio vilivyo nje ya hifadhi na hata kuminya fursa kwa maeneo ya jirani na hifadhi kujitangaza zaidi.
Katika kukabiliana na sintofahamu ya sheria hii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, akiwa mkoani Simiyu hivi karibuni alitoa maagizo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Bodi ya Utalii, kuangalia upya sheria zilizopo kwa kuondoa utaratibu unaowazuia watalii kutotoka ndani ya hifadhi mpaka wanapomaliza siku walizolipia.
Kanyasu alisema utaratibu huo ni chanzo cha kutokujulikana kwa vivutio vya utalii katika maeneo mengine yanayopakana na hifadhi za taifa na pia huwanyima watalii fursa ya kujifunza utamaduni wa makabila ya maeneo hayo kama vile ngoma, mavazi na vyakula kutokana na sheria kutowaruhusu wao kutoka ndani ya hifadhi hadi pale watakapokamilisha ziara yao.