TUNU NASSOR NA HERIETH FAUSTINE
-DAR ES SALAAM
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakusudia kufuta umiliki wa shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33 lililopo Mabwepande mkoa wa Dar es Salaam.
Hatua ya kufutiwa umiliki wa shamba hilo imetokana na agizo la Rais Dk.John Magufuli la kutaka maeneo yote ambayo hajaendelezwa na wamiliki kunyang’anywa na kugawiwa kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli iliwachochea wananchi zaidi ya 100, wakiwamo waliobomolewa nyumba maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, kulivamia shamba Sumaye na kujikatia viwanja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi alisema tayari wametoa notisi ya siku tisini ya kulifutia hati shamba hilo kutokana kukaa muda mrefu bila kuendelezwa.