29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SHAMBA LA KAPUNGA NA KITATANGE KWA WANANCHI

Na Bakari Kimwanga-Aliyekuwa Mbarali



NENO kitatange kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili ni samaki mdogo wa umbo la duara, mwenye rangi ya manjano iliyochanganyika na nyeupe na pezi lililotanda mgongo mzima, mwenye tabia ya kuwasakiza wenziwe kwenye mtego kama vile dema, kisha yeye akatoka.

Hata katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, mojawapo ya mambo yalitengenezewa mchakato mahsusi katika kupata suluhu ya matatizo ya ardhi lakini wajanja wachache hutumia fursa hiyo kwa kujinufaisha.

Baada ya kutungwa kwa sheria mpya za ardhi mwaka 1999, yaani Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya ardhi pia umebadilika.

Miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanywa na sheria hizi, ambazo ni matokeo ya sera ya ardhi ya Taifa ambao unatengeneza mfumo wa kipekee wa kutatua matatizo ya ardhi.

Sehemu ya tano ya sheria ya ardhi ya vijiji, namba 5 ya mwaka 1999, inahusu utatuzi wa migogoro ya ardhi ya kijiji.
Pamoja na sheria hiyo sasa kutimia miaka 15 tangu zilipoanza kutumika kwa baadhi ya maeneo imekuwa ni kama kitanzi kwa Watanzania hasa wanaoishi maeneo ya vijijini kujikuta wakichukuliwa ardhi yao kwa kile kinachoitwa uwekezaji.

Januari 5, mwaka 2016, Rais Dk. John Magufuli, alimaliza sehemu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited na sasa hekta 1,780 zitakuwa mali ya wananchi.
Kijiji cha Kapunga kina wananchi 4,500 ambao asilimia 95 huendesha maisha yao kwa kazi ya kilimo cha mpunga na mazao mengine mchanganyiko yakiwemo mahindi.

Mwaka mmoja na nusu sasa tangu Serikali ilipotangaza uamuzi huo ambapo sasa ni wazi matokeo ya uwekezaji wa uhakika unaanza kuonekana katika kijiji hicho.

Shamba la Kapunga lilibinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya “Export Trading,” ya jijini Dar es Salaam mwaka 2006 katika kile kilichoelezwa kuwa ni hatua muhimu ya kulifufua shamba hilo ambalo awali lilimilikiwa na Serikali.

Kabla ya kuuzwa, shamba hilo lilitumiwa na wakulima wadogo waliokuwa wakilima kwa kukodi ambapo walifanikiwa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani sita kwa hekta.

Pamoja na mafanikio hayo ya wakulima wadogo na ombi lao la kulinunua shamba hilo hata kwa shilingi bilioni kumi, walipuuzwa na hatimaye kuliuza kwa kampuni hiyo kwa gharama ya Sh bilioni 2.5.

 

USHIRIKISHWAJI WANANCHI

Baadhi ya halmashauri zimekuwa haziwashirikishi wananchi vya kutosha katika mipango ya uendelezaji wa ardhi yao na hivyo kusababisha migogoro wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo.

Ingawa Sheria inatamka wazi kuhusu umuhimu na hatua za kuwashirikisha wananchi, baadhi ya halmashauri hupuuza ushirikishwaji huo na mwishowe hupata ugumu kwenye utekelezaji na pengine kusababisha migogoro mikubwa.

Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 ni Sera ya msingi inayotoa dira ya Serikali katika usimamizi wa ardhi nchini. Pamoja na Sera hii, ipo Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 inayotoa dira ya Serikali kuhusu maendeleo ya makazi.

MGOGORO ULIPOANZA

Pamoja na kurejeshwa kwa ardhi hiyo lakini wananchi wa kijiji hicho bado wanaamini kuwepo kwa udanganyifu katika utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu hekta 1,870.

Wanadai kwamba, maofisa watatu wa ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na mmoja kutoka ofisi ya Kamishna wa ardhi mkoani Mbeya, wanatuhumiwa na wananchi hao kuwa nyuma ya udanganyifu huo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kapunga wakati wa vikao hivyo, Ramadhan Nyoni, anasema katika kikao waliigomea ramani iliyotolewa na wataalamu hao wa ardhi na kukubaliana mwekezaji kuachiwa hekta 5,500 kama ilivyo katika ramani halisi ya shamba hilo huku hekta 1,870 alizozidishiwa, zirudishwe kwa wananchi.

Licha ya hali hiyo, bado anashukuru sehemu ya ardhi hiyo kurejeshwa kwa wananchi ili kuruhusu shughuli za maendeleo kwa uhakika kuliko ilivyokuwa awali.

UPANGAJI WA ARDHI

Jackson Mbilinyi ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kapunga, anasema baada ya kurejeshwa kwa ardhi hizo, Serikali ya kijiji ilifanya mkutano na wananchi Februari mwaka huu na kuamua kwa pamoja hatima ya ardhi hiyo.

“Tulikubaliana katika mkutano wetu kwamba, viwanja 250 vyenye ukubwa wa 35 kwa 35 vitagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi hasa katika kitongoji cha Mapogoro na Ofisini.

“Na viwanja hivi vitagawiwa kwa shilingi 100,000. Licha ya hali hiyo pia tulitenga viwanja 60 vyenye ukubwa wa ekari moja kwa ajili ya uwekezaji ambapo kila kimoja kitapatikana kwa gharama ya Sh milioni mbili. Hata hivyo, tulifanya tena marekebisho na kushusha na gharama sasa ni shilingi milioni moja,” anasema Mbilinyi.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kapunga, Brighton Mwinuka, anasema licha ya wataalamu wa Serikali kupima shamba hilo na kurejeshwa sehemu ya ardhi, lakini bado wanaona wanahitaji kufanya uhakiki wa wazi wa mipaka ya shamba hilo.

“Kwa mujibu wa Serikali ni kwamba, huu mgogoro umekwisha na sasa tunatakiwa kusonga mbele, suala la uhakiki wa mipaka ni muhimu maana bado wananchi wangu hawana imani hasa katika ukubwa uliotolewa wa shamba hili.
“Tunahitaji kuwa na mardhiano ya pamoja kuliko ilivyo sasa,” anasema Mwinuka.

 

KAULI YA KAPUNGA

Uongozi wa Shamba la Kapunga unatofautiana na wanakijiji cha Kapunga, unaamini kuwa mchakato wa kuondoa hekta 1,870 ulifanyika na iwapo kutakuwa na udanganyifu wowote basi hilo si tatizo lao bali ni la Serikali.
Ofisa Mwajiri wa Shamba la Kapunga, James Maliki, alinukuliwa akisema suala la mipaka lilikamilika na wanakijiji cha Kapunga walikabidhiwa ardhi yao.

Maliki anawashutumu Serikali ya Kijiji cha Kapunga na viongozi wake akisema waligoma kushirikiana na wapimaji walipofika kuweka mipaka mipya ya shamba hilo. Kwa mujibu wa Ofisa Mwajiri huyo, wapimaji waliondoa hekta 1,870 kutoka shamba la Kapunga na kukabidhi kwa kijiji hicho, jambo ambalo linapingwa vikali na wanakijiji.
“Kama ni udanganyifu hilo halituhusu, ni Serikali iliyopima, tatizo ni Serikali ya kijiji na viongozi wake,” anasema Maliki.

 

KILIO CHA WANANCHI

Sekelaga Mwandubya ni mmoja wa wanawake wanaoishi katika Kijiji cha Kapunga, anasema kwa sasa mgogoro huo umekwisha ila kilichobaki ni kuondolewa kwa kero ndogondogo hasa ya namna bora ya kutumia maji ambayo mwekezaji anadai yeye ndiye mwenye haki.

“Ni vema Serikali sasa iingilie kati suala la matumizi ya maji kwani kwa sasa tunashindwa kutokana na mwekezaji kudai yeye ndiye mwenye haki ya maji hata yale tunayopata ni kidogo sana na suala hilo hata uongozi wa halmashauri unajua,” anasema Sekelaga.

 

MSIMAMO WA SERIKALI
Akizungumzia madai hayo Kaimu Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Mbarali, Geofrey Mwaijebele, anasema hatua iliyofikiwa na Serikali inakamilisha mchakato wa mgogoro wa shamba hilo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Anasema baada ya uamuzi wa Serikali suala la mamlaka ya ardhi hiyo yapo kwa Serikali ya kijiji ambayo ndiyo inapaswa kuisimamia ardhi hiyo kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya Ardhi ya mwaka 1999.

“Baada ya uamuzi wa Rais Dk. Magufuli, kwa mujibu wa sheria suala la ardhi sasa limerudi kwa Serikali ya kijiji wao ndio wanaojua nani amepewa ama la. Ingawa Kapunga ya sasa si ile ya zamani ambapo inaonekana wazi hata shughuli za uwekezaji zimeshika kasi ikiwemo ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia mazao pamoja na kituo cha mafuta.

“…na hili linatokana na uwepo wa uhakika wa uwekezaji katika kijiji hicho ambapo awali kila mmoja alikuwa akihofia hata kujenga nyumba nzuri au kufanya uwekezaji wowote.
“Si hilo tu katika kile kinachoitwa ujirani mwema mwekezaji ameweza kutenga hekta 50 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kisasa ambapo baada ya kukamilika kwake kwa mujibu wa mkataba itarejeshwa katika mikono ya wananchi wenyewe kupitia Serikali ya Kijiji,” anasema Mwaijebele.

 

MAMLAKA YA MAJI

Kutokana na mgogoro huo wa haki ya kutumia maji, Msimamizi wa Ofisi ndogo ya Bonde la Mto Rufiji iliyopo Mbarali, Abisai Chilunda, anasema tayari wamepokea malalamiko ya wakulima wadogo kuhusu nani mwenye haki ya kutumia maji.

“Kibali cha maji kilitolewa kwa mwekezaji wa Kapunga ambaye alipewa kutumia maji lita za ujazo 1,000 kwa sekunde lakini mahitaji ni zaidi ya hayo. Hivyo baada ya wananchi kuwa na umiliki halali wa ardhi yao tumewataka waombe kibali ili na wao wawe na haki ya kutumia maji hayo.

“Tayari tumeshapokea maombi yao na wakati wowote bodi itakutana na kufanya marekebisho ya kibali hiki cha haki ya kutumia maji kutoka Mto Ruaha Mkuu ambao husimamiwa na Bonde la Mto Rufiji,” anasema Chilunda

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles