Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Zaidi ya Sh bilioni 20 zimekusanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) tangu lilipoanza kutoa huduma za kusafirisha abiria kupitia treni ya kisasa ya SGR.
Safari za treni hiyo zilianza rasmi Julai 14,2024 kwa Dar es Salaam na Morogoro kisha baadaye kuongezwa za Dar es Salaam na Dodoma.
Akizungumza leo Novemba 14,2024 baada ya kutembelea shirika hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustino Vuma, amesema wameridhika na hali ya uendeshaji wa treni hiyo.
“Mapato yatokanayo na abiria huwa ni asilimia ndogo lakini asilimia 80 na zaidi mara nyingi inatokana na usafirishaji wa mizigo, kama haya yaliyopatikana ni asilimia 20 tunaamini mizigo ikianza wafanyabiashara wengi watatumia fursa hiyo na mapato ya shirika yataongezeka,” amesema Vuma.
Kamati hiyo pia imelishauri shirika hilo liendelee kuweka teknolojia zaidi za ulinzi na kuwachukulia hatua kali watu wanaohujumu miundombinu ya reli hiyo.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema watahakikisha wanamalizia vipande vilivyobaki ili shirika liendelee kunufaika kwa kubeba abiria na mizigo wapate faida kubwa kama nchi.
“Kamati imeridhika kwamba uwekezaji uliofanywa katika sekta hii una tija kubwa kwa taifa letu kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo, tutafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ili shirika liendelee kunufaika,” amesema Kihenzile.
Amesema Serikali inajenga reli hiyo kutoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma kilomita 2,300 na kwamba hadi sasa Sh trilioni 27 zimewekezwa kwenye mradi huo.
Kuanzia mwakani shirika hilo linatarajia kuanza kusafirisha mizigo kwenye reli hiyo hatua itakayowezesha mapato kuongezeka zaidi.