*Yaipongeza BRELA kwa kuendelea kutoa elimu
Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuzibaini kampuni zote ambazo zinafanya kazi bila kusajiliwa sambamba na kwenda kinyume na sheria za nchi.
Aidha, imezitaka benki nchini kusaidia kutoa taarifa za wamiliki wa kampuni ambao taarifa zao haziko wazi ikiwamo kukiuka maadili.
Hayo yamebainishwa leo Juni 27, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, katika warsha ya uhamasishaji wadau kuhusu kanuni za wamiliki manufaa iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni–BRELA na kuwakutanisha Chama cha mabenki nchini.
Kwa mujibu wa Mpogolo, mwaka 2020 kupitia sheria ya makampuni Serikali imefanya marekebisho mbalimbali ikiwemo kuongeza kipengele cha umiliki manufaa ili kuzifanya kampuni zote ambazo zimesajiliwa hapa nchini kutambulika huku akisema sheria hiyo haijalenga kumkandamiza mwekezaji.
“Jitihada hizi za Brela za kuunga mkono juhudi mbalimbali za Serikali haziwezi kufanikiwa bila kushirikiana na mabenki, ninyi ni watu muhimu sana, BRELA ni kiungo kati ya maelekezo, maagizo na sheria mbalimbali za serikali lakini watekelezaji mnajikuta ni ninyi watu wa benki moja kwa moja, hivyo ili kufanikiwa tunawahitaji sana tushirikiane.
“Yapo makampuni ambayo tayari yamepata mwitikio huu, hivyo niwasihi baada ya mafunzo na elimu hii twendeni tukayafichue makampuni ambayo tunajua bado wamiliki wake hawajaweza kufahamika, ili taarifa zake ziweze kufahamika vizuri,” amesema Mpogolo na kuongeza kuwa:
“Thamani ambayo mmeipa Brela ni kwa mujibu wa sheria ambayo imetungwa na bunge kwani bila thamani hiyo na sisi tusingeiona, tunawaona kama sehemu ya lulu ya mafanikio ya awamu ya sita, kwani tukiweza kuiishi hii sheria tutatimiza malengo ya serikali,” amesema Mpogolo huku akiipongeza BRELA kwa kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali.
Upande wake, Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa amesema wameona kuna umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa kuwashirikisha wadau kutoka kwenye sekta ya Benki.
“Hii ni baada ya mabadiliko ya sheria yaliyopitishwa na Bunge la Tanzania na kupitishwa kwa kanuni za Umiliki Manufaa na Waziri mwenye dhamana ya Biashara imeonekana ni muhimu sana kutoa elimu hii kwa wadau tunaofanya kazi kwa pamoja.
“Kupitia warsha hiyo itaibua michango mizuri na kuwezesha kuwa na uelewa wa pamojaambao utasaidia kufanikisha zoezi hilokwa manufaa ya wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla,” amesema Mkapa na kuongeza kuwa:
“Warsha hii ni kwa ajili ya taasisi za kifedha ili kuelimishana na kukumbushana juu ya mabadiliko haya na hatimaye kupata uelewa wa pamoja utakaowezesha kufanya kazi hizi kwa ufanisi zaidi,” amesema Mkapa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara–BRELA, Isdor Nkinda amesema uwasilishaji wa taarifa wa umiliki manufaa ni takwa kisheria huku yeyote atayakae toa taarifa za uongo adhabu yake ni kifungo au faini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Tusekelege Joune amewashukuru BRELA kwa kuandaa warsha hiyo kwani ni sehemu moja wapo ya kuwapa mwanga watu wa benki ili waweze kuelewa juu ya hiyo sheria na ni kwa namna gani anapaswa kutafuta taarifa za mmiliki wa kampuni.
“Tumekuwa mstari wa mbele na nijukumu letu kisheria kusaidia kutoa taarifa zozote ambazzo aidha zina mashaka au siyo za kawaida, pia tunatakiwa kujua mtu tuliyemfungulia akaunti kwani ni moja wa sehemu tunayosema kwamba mjue mteja wako, hivyo kupitia sheria hii ya BRELA itatusaidia kujua nani ni nani katika kampuni husika,” amesema Joune.
Kwa kipindi kirefu sasa BRELA imeendelea kukutana na makundi mbalimbali katika jamii kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu mabadiliko mbalimbali yakiwamo ya sheria.