26.1 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yazindua Nembo ya Uhuru

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Serikali imezindua rasmi nembo na kaulimbiu ya maadhimisho ya sherehe ya miaka 60 ya Uhuru zitakazofanyika Desemba 9, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Saalam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo, Jumatatu Novemba mosi 2021, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana Ajira na Wenyeulemavu), Jenista Mhagama, amesema kutokana na umuhimu wa maadhimisho hayo mwaka huu serikali imeazimia kuwa na shughuli zitakazofanyika maeneo mbalimbali ya nchi.

“Lengo ni kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea na hasa mafanikio tuliyopata yanayoonyesha dhahiri maendeleo ya miaka 60, ya uhuru wa nchi yetu na watu wake,” amesema Mhagama.

Amesema shughuli za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru zitahusisha Wizara na Taasisi zote za serikali kuelezea hatua ambazo kila sekta imepiga tangu Uhuru, tuliposasa na tunapoelekea.

Waziri Mhagama amesema ratiba ya mikutano ya Mawaziri na vyombo vya habari kuhusu historia ya nchi tangu ilipotoka uhuru hadi sasa kwa kila sekta itaanza Novemba 2, Mwaka huu ambapo itaratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO kwa kushirikiana na sekta husika.

Pia amesema kutakuwa na mahojiano maalum kati ya vyombo vya habari na viongozi mbalimbali wa serikali walioko madarakani na wastaafu, watu mashuhuri, sekta binafsi na wananchi.

Amesema Mahojiano hayo yatahusisha viongozi na wananchi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Vilevile amesema   maadhimisho hayo yatahusisha mashindano ya insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, michezo kama mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha na mashindano ya baiskeli.

Pia kutakuwepo na maonyesho ya sanaa na ngoma za jadi, Makongamano ya Kikanda na Kitaifa, Mdahalo wa kitaifa, Maonesho ya Maalum ya Vijana kuonesha Ubunifu na ujuzi katika sekta mbalimbali pamoja na Maonesho ya Biashara ya Kitaifa yatakayotanguliwa na Mkutano wa uwekezaji.

Amesema  matukio hayo yatafanyika katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia leo  hadi Novemba 30, 2021.

Amesema Disemba 2, 2021 utafanyika uzinduzi rasmi wa Juma la Kilele cha sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

“Uzinduzi huu utafanyika Jijini Dodoma na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesema Mhagama.

Amesema kuwa pia kutakuwepo na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya Maendeleo itakayozinduliwa na viongozi wa Kitaifa wakiwemo wa mihimili ya Bunge na Mahakama wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa kutakuwa na mkutano wa uwekezaji ambao utafuatiwa na maonesho ya kitaifa ya biashara utakaojumuisha wafanyabiashara wa pande zote mbili za Muungano.

“Mkutano na Maonesho hayo yatafanyika Zanzibar kuanzia Desemba 3, 2021 na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles