30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatumia Sh trilioni 22 hadi machi 2020

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA

SERIKALI imesema hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya shilingi trilioni 22.65 zimetolewa kugharamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 33.98 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 18 ya kimkakati.

Pia inakamilisha uchambuzi wa taarifa mbalimbali za kisekta ili kubaini kiwango cha athari zitokanazo na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Hayo yalielezwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2020-2021.

Wizara ya Fedha na Mipango inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi trilioni 12.39 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 11.73 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 659 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Katika mwaka 2019/20, Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi trilioni 11.94 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo

Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 11.21 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 730.58 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Hivyo bajeti ya Wizara hiyo imeongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni 1.

UFAFANUZI WA TRIL. 24

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Mpango alisema hadi kufikia Machi 2020, jumla ya shilingi trilioni 24.65 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Alisema katika kipindi hicho, shilingi trilioni 1.16 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo na shilingi bilioni 597.54 kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa ya wakandarasi (shilingi bilioni 247.50), wazabuni (shilingi bilioni 147.73), watumishi (shilingi bilioni 97.62), madeni mengineyo (shilingi bilioni 88.87) na watoa huduma (shilingi bilioni 15.82). 

Aidha, jumla ya shilingi bilioni 33.98 sawa na asilimia 84.95 ya bajeti iliyotengwa zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 18 ya kimkakati inayotekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

MAKUSANYO BILIONI 626.57

Waziri huyo alisema katika mwaka 2019/20, Wizara ilikadiria kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 967.04 kutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwemo gawio, kodi za pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma, mauzo ya leseni za udalali na nyaraka za zabuni. 

Alisema hadi kufikia Machi 2020, Wizara imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 626.57 sawa na asilimia 64.79 ya lengo.

USIMAMIZI WA BAJETI ILIYOPITA

Waziri Mpango alisema katika mwaka 2019-2020, Wizara ilipanga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato. Alisema Sera na mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi, kuhimizi matumizi ya Tehama katika usimamizi wa kodi, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika za Taasisi za Umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache ili kuhakikisha kuwa michango stahiki ya taasisi za umma inawasilishwa kwa wakati.

Pia kuhakikisha kuwa maduhuli yote yanakusanywa kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG).

Alisema hatua hizi, pamoja na nyingine za usimamizi wa mapato, zimeiwezesha Serikali kukusanya mapato ya ndani jumla ya shilingi trilioni 16.06 katika kipindi cha Julai 2019 na Machi 2020 sawa na asilimia 92.4 ya lengo.

Alisema kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yalifikia shilingi trilioni 13.46 sawa na asilimia 94.7, mapato yasiyo ya kodi shilingi trilioni 2.07 sawa na asilimia 84.4 na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi bilioni 527.3 sawa na asilimia 91.7.

Alisema Mapato ya Ndani yameongezeka kwa asilimia 14.2 hadi shilingi trilioni 16.06 kutoka shilingi bilioni 14.07 kwa kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

DENI LA TAIFA

Waziri Mpango alisema Wizara inaendelea kusimamia Deni la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada.

Alisema Kipaumbele ni kukopa kutoka kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu na fedha zinazopatikana kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hususan miradi inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya watu.

Vile vile, Wizara inaendelea kuhakikisha kuwa, madeni yote yanayoiva yanalipwa kwa wakati. 

Waziri huyo alisema hadi kufikia mwezi Machi 2020, Serikali ilifanikiwa kulipa deni lake lote lililoiva lenye thamani ya shilingi trilioni 6.19.

Alisema kati ya kiasi hicho, Deni la Ndani ni shilingi trilioni 4.06 ikijumuisha riba shilingi 22 trilioni 1.08 na mtaji shilingi trilioni 2.98. 

Aidha, Deni la Nje ni shilingi trilioni 2.13 ikijumuisha riba ya shilingi bilioni 636.75 na mtaji shilingi trilioni 1.49.

MAFAO YA WASTAAFU NA MIRATHI

Waziri huyo wa Fedha na Mipango alisema kati ya Julai 2019 na Machi 2020, Wizara imelipa mafao na pensheni kwa wastaafu wa Serikali 57,605, mirathi kwa warithi 1,006 na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi 457 wa Serikali walio kwenye mikataba.

Aidha, Wizara imeendelea kufanya uhakiki wa Daftari la Pensheni kila mwezi kabla ya malipo, kuandaa vitambulisho vipya vya wastaafu vya kielektroniki katika mfumo wa “smart cards” na kuboresha mfumo unaotumika kutoa huduma kwa njia ya mtandao na kudhibiti fedha za mirathi zinazotoka Hazina kwenda moja kwa moja kwenye akaunti za warithi.

UDHIBITI NA UTAKATISHAJI FEDHA

Waziri Mpango alisema Kitengo cha Udhibiti Fedha 30 Haramu kilipokea na kuchambua taarifa za miamala shuku 724 kati ya Julai 2019 na Machi 2020.

Alisema kati ya miamala hiyo, taarifa fiche 61 zimewasilishwa kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria kwa ajili ya uchunguzi.

 Serikali yatumia Sh trilioni 22

Aidha, Kitengo kimeingia makubaliano na Vitengo vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Japan kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati ya kimataifa ya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

CHANGAMOTO

Alisema wanakabiliwa na changamoto za kasi ndogo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pia Mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia ya mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato yanayoleta uhitaji wa upatikanaji wa teknolojia mpya na kuboresha na kuhuisha teknolojia ya mifumo iliyopo ili kuongeza ufanisi.

“Kuongezeka kwa gharama za mikopo kwenye masoko ya fedha duniani kutokana na mabadiliko ya sera za fedha katika nchi zilizoendelea (hususan Marekani na Nchi za Ulaya),”alisema.

Alisema Wizara inakamilisha uchambuzi wa taarifa mbalimbaliza kisekta ili kubaini kiwango cha athari zitokanazo na mlipuko virusi vya corona katika uchumi na kuainisha mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kukabiliana nazo.

KITUO CHA UBIA KUANZISHWA

Alisema katika mwaka 2020/21, Wizara inatarajia kukamilisha taratibu za kuanzisha kituo cha ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – PPP Center.

Aidha, Wizara itaendelea kupokea na kufanya upembuzi yakinifu wa miradi ya ubia itakayowasilishwa na Taasisi na Mashirika ya Umma na kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa wadau wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.

UKUAJI WA MIKOPO SEKTA BINAFSI

Vile vile, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020 ulifikia asilimia 9.0 ikilinganishwa na asilimia 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles