Hadija Omary, Lindi
Serikali siku 14 kwa kampuni au taasisi zinazomiliki viwanda vilivyobinafsishwa na serikali bila kuviendeleza ama kubadilisha matumizi viwanda hivyo, kuwasilisha mipango mikakati yake kwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ya kuviendeleza viwanda hivyo kabla ya serikali haijachukua hatua nyingine dhidi yao.
Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda amesema hayo alipofanya ziara ya siku moja mkoani Lindi ambapo pamoja na mambo mengine, amekagua kiwanda kinachotarajiwa kubangua korosho cha Bucco kilichopo Manispaa ya Lindi pamoja na ghala la kuhifadhia mazao la Ilulu wilayani Nachingwea.
“Katika kulisimamia jambo hilo kama wizara tayari nimeshamuagiza Katibu Mkuu kuandaa taarifa ya uchambuzi kwa nchi nzima ili kubaini viwanda vyote vidogo, vikubwa na vya kati kwa vile vilivyobinafsishwa ili kubaini kama vinafanya kazi yake ya msingi iliyokusudiwa.
“Baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa wizarani itapitiwa ili kuona ni viwanda vipi vinafanya kazi iliyokusudiwa na vipi vilivyobadilishwa matumizi kwa vile vitakavyobainika kuwa vimebadilishwa matumizi ama kutoendelezwa hatua za haraka zitachukuliwa na serikali,” amesema.
Akizungumzia juu ya urejeshwaji wa kiwanda cha Bucco, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, amesema serikali ilipoamua kiwanda hicho kukikabidhi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , nia ilikuwa ni kuiongezea thamani korosho ndani ya nchi kutoka moja kwa moja kwa wakulima ambapo inaweza kukuza pato la taifa pamoja na kuleta ajira kwa wananchi.