31 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa neno mkataba wa TICTS

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Siku chache baada ya kuwapo kwa mapendekezo ya wadau mbalimbali kikiwamo chama cha ACT Wazalendo kutaka kutokuongezewa tena mkataba kwa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Shehena za Kontena Bandarini (TICTS), Serikali imesema ipo kwenye mazungumzo na kampunihiyo ili kuona kama wanaweza kuwaongezea mkataba au la.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Agosti 4, 2022 Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akitoa utaratibu na mtazamo wa utekelezaji wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Profesa Mbarawa amesema TICTS inafanya kazi kisheria kwa kuwa kuna mkataba kati yake na serikali ambao utaisha mwezi ujao.

Amebainisha kuwa kwenye mkataba huo kuna mambo mengi yaliyozungumzwa na kwa sasa kuna mazungumzo yanayoendelea baina ya pande hizo mbili.

“Sasa kama tutaongeza mkataba au hatuongezi, hapa siyo mahali pake, siku ikifika tutawaita na tutawaeleza kwa nini tumeongeza au kwa nini hatukuongeza.

“Kitu ambacho kimetokea kwenye ule mkataba wenyewe ni kwamba mkiweka mkataba kunakuwa na vigezo ambavyo mnaweka, vigezo vilivyowekwa ukiangalia vingine pengine vimetimizwa au havikutimizwa, kuhusu magari kuchelewa kutoka sijui kama hicho kigezo kipo kwenye mkataba au hakipo,” amesema Prof. Mbarawa.

Amefafanua zaidi kuwa magari kuchelewa kutoka bandarini kunachangiwa na mambo mengi ikiwamo mizani iliyokuwapo ya kupima mizigo inayotoka na pia baadhi ya watu walikuwa wanapeleka kuegesha magari yao siku mbili kabla ya kupakia mzigo hali iliyochangia kuwepo kwa foleni.

“Bandarini siyo mahali pa watu kwenda kulala, ilifika mahali unakuta madereva pale wamelala tu, matokeo yake wanasababisha foleni kubwa, tukasema hapana,” amesema Prof. Mbarawa.

Akizungumzia juu ya mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, amesema serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) inatekeleza kazi ya kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli hadi kufikia mita 15.5 kutoka mita 12 imefikia asilimia 48.

Amefafanua kuwa serikali inafanya hivyo kwa sababu meli kubwa za kisasa zinahitaji kina kikubwa ili ziweze kuingia bandarini kwa urahisi, nakwamba kinyume na hivyo vyo meli zitakwenda kwenye bandari za nchi jirani.

Amesema kwa umuhimu huo, ndipo serikali iliamua kufanya maboresho makubwa bandarini ikiwamo kufanya ukarabati wa gati namba nane hadi 11 kwa kuongeza kina kutoka mita 11 za sasa hadi mita 14.5.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, TPA imetengewa shilingi bilioni 100 fedha za nje kutoka Benki ya Dunia na shilingi bilioni 650 kutoka vyanzo vya ndani vya mapato vya mamlaka kwa ajili ya kutekeleza miradi,” amesema Prof. Mbarawa.

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni kuongeza kina na kupanua lango la kuingilia na kugeuzia meli; kuboresha gati namba nane hadi 11; gati namba 12 hadi 15; kufunga na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na mifumo ya Tehama; kuboresha Bandari ya Tanga awamu ya pili kwa kujenga gati namba 1 na 2 zenye jumla ya urefu wa mita 450.

Aidha, kuhusu madai kwa kampuni inayofanya uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuidai serikali takribani Sh bilioni moja kutokana na ucheleweshaji wa mradi, amesema serikali haidaiwi fedha yoyote na Kampuni ya China Harbour kwa kuwa fedha zipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles