Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
SERIKALI imewataka wananchi kuacha kutumia kiholela dawa za ‘antibiotic’ ili kuepuka usugu wa vimelea unaosababishwa na matumizi yasiyofaa ya dawa hizo.
Miongoni mwa dawa ambazo zimetolewa tahadhari ni pamoja na za pneumonia, UTI, fungus, kifua kikuu na nyingine ambazo usugu umefikia asilimia 44 kwa mikoa yote.
Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Usugu wa Vimelea Utokanao na Dawa Novemba 18 hadi 24, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi alisema ni muhimu wananchi kufuata masharti ya matumizi ya dawa ili kuokoa maisha yao na gharama za matibabu.
“Tunaanza wiki ya maadhimisho ya kuhamasisha wananchi kuhusu uelewa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali zinazojulikana kama antimicrobials (antibiotic) zinazotumika kutibu magonjwa kama pneumonia, UTI, fungus, TB na mengine.
“Tunachokihamasisha kwa wananchi wawe waangalifu katika kutumia hizi dawa, wazitumie kwa usahihi ili tuepuke usugu wa vimelea.
“Wananchi wanapoenda kwenye maduka wapewe dozi wanazoweza kutumia kwa muda ambao unatakiwa kama ni siku tano, saba ama 10.
“Kwahiyo tunaomba wananchi wafuate masharti ya utumiaji wa dawa kulingana na madaktari wanavyowaeleza, wasijichukulie dawa hovyo,” alibainisha Profesa Makubi.
Pia alitoa wito kwa wenye maduka ya dawa waache kutoa dawa bila mgonjwa kuwa na risiti au cheti cha daktari.
“Tayari sasa tuna sheria ambayo inadhibiti hawa wauza dawa ambao wanatoa dawa kiholela kwa kutaka kujiongezea kipato bila kufuata taratibu au bila kusubiri daktari aandike cheti.
“Wananchi waelewe wasikubali kupewa dawa tu anapoenda kwenye duka na wanaweza kuripoti katika vyombo vya sheria.
“Tuondokane na kutumia dawa zetu kiholela kwa sababu italeta usugu mkubwa wa kuangamiza taifa na kuleta hasara kwa kutumia mabilioni ya fedha ya kutafuta dawa zingine zenye gharama kubwa kwa ajili ya kutibu wananchi,” alisema Profesa Makubi.
Alisema usugu wa vimelea unatofautiana kulingana na aina ya dawa, huku akitolea mfano dawa za kifua kikuu kwamba mgonjwa anapoenda mara ya kwanza kuanza dawa tayari asilimia moja wana usugu wa dawa.
“Lakini kwa wanaorudi baada ya kuugua ukiangalia makohozi yao au ukatumia njia nyingine karibu asilimia nne wana usugu wa dawa za TB.
“Ukija kwenye malaria tukaenda kwenye klorokwin ilifikia kiwango cha usugu wa asilimia 50 kwa wananchi, tukaja ASP ikaonekana ina usugu mkubwa tukaondoa kabisa, kiwango kilizidi asilimia 50.
“Dawa za UTI pia zina usugu, kama za centriacson imeshafika asilimia karibu 44 baadhi ya mikoa, hizi ni dawa zinazotumika kutibu kwa njia ya sindano kwenye UTI, Pneumonia na magonjwa mengine.
“Usugu unabadilika kulingana na dawa, lakini kwa viwango tofauti tofauti, hiyo ni hatari, ikifika asilimia 50 inaweza kuondoa hiyo dawa sokoni,” alisema Profesa Makubi.
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema adhabu zinazoweza kutolewa kwa wakiukaji wa sheria ni pamoja na kupigwa faini ya papo kwa papo, kifumgo cha miezi sita hadi mwaka mmoja na nusu.
“Kuna uwezekano wa kupoteza biashara kwa kufungiwa, yote yameainishwa kulingana na unavyokiuka hizo taratibu, na kanuni za udhibiti wa uuzaji wa dawa imeshasainiwa mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka 2020. Tayari taratibu za kuwajibisha watu zinaendelea na matumizi yake yameanza rasmi.
“Tunaimarisha vitengo vya ukaguzi kupitia Baraza la Famasi, tutakasimisha baadhi ya majukumu kwenye halmashauri na mikoa ambako kuna watu wengi, kuhakikisha kanuni zinafuatwa,” alisema Msasi.
Mwakilishi wa mkurugenzi wa huduma za mifugo, Dk. Gibonce Kayuni aliwataka wafugaji waepuke kutoa dawa kwa wanyama bila kufuata ushauri wa wataalamu wa mifugo.
“Tunawaomba wafugaji wasichinje mnyama anayeendelea na dozi kwa sababu madhara yanaenda kwa walaji, ng’ombe akitumia dawa akafa wasitumie nyama yake, watumie wataalamu wanaotambulika kutibu wanyama, wawe wanaenda dukani kununua dawa kwa kujua matumizi sahihi,” alishauri Dk. Kayuni.