30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yashauriwa kuipa kipaumbele elimu ya awali

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imeshauriwa kuipa kipaumbele elimu ya awali kwa kuhakikisha watoto wote wanaotakiwa kusajiliwa katika shule za awali wanasajiliwa ili kuandaa taifa litakalokuwa na ujuzi na maadili mema.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Alluminium, John Ryoba, wakati wa mahafali ya kwanza ya Shule ya kulelea watoto ya Chadash iliyopo Kibaga B Kata ya Kinyerezi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Alluminium, John Ryoba, akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya Shule ya Chadash iliyopo Kibaga B Kata ya Kinyerezi.

Amesema elimu ya awali ni ngazi ambayo kama Serikali itawekeza vya kutosha inaweza kutengeneza taifa ambalo halina mmonyoko wa maadili kama watumiaji wa dawa za kulevya au wezi.

“Tunawekeza zaidi kwenye elimu ya juu, sekondari na msingi lakini tunasahau elimu ya awali, ndiyo maana mtu unajenga nyumba unaipaka rangi inaonekana nzuri lakini msingi wake ni mbovu ikija mvua jengo linadondoka.

“Hivyo naiomba Serikali katika kila shule ya msingi itenge darasa moja kwa ajili ya elimu ya awali ili kuandaa vijana watakaokuja kuliendesha taifa kwa kuwa na misingi imara ya elimu na maadili,” amesema Ryoba.

Aidha amempongeza mkurugenzi wa shule hiyo kwa kuamua kuwekeza katika elimu na kumtaka awekeze zaidi hadi elimu ya juu.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibaga, Hashim Gulana, amesema mtaa huo wenye wakazi zaidi ya 10,000 kwa sasa una shule tano na kati ya hiyo mbili ni za serikali na tatu za binafsi.

“Idadi ya watu katika mtaa wetu inaongezeka siku hadi siku hivyo, tunahitaji uwekezaji mkubwa katika shule kukidhi ongezeko la watu,” amesema Gulana.

Aidha ametoa wito kwa wazazi kuendeleza maadili mema wanayopata watoto kutoka katika shule na vituo mbalimbali huku akiahidi kusaidia sare na vifaa vya shule kwa wazazi watakaokwama ili kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule.

Wanafunzi wa Shule ya Chadash wakicheza wakati wa mahafali ya kwanza yaliyofanyika shuleni hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Chadash, Kokwihukya Kaino, amesema ilianzishwa Novemba mwaka 2020 na mpaka sasa imefanikiwa kununua gari la shule kurahisisha usafiri wa kuwaleta na kuwarudisha wanafunzi na kuongeza eneo kwa lengo la kutoa elimu hadi ya msingi.

Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara hasa wakati wa mvua, baadhi ya wazazi kutolipa ada na michango mbalimbali kwa wakati hali inayokwamisha uendeshaji wa shule na baadhi ya wanajamii kutoelewa umuhimu wa malezi ya watoto shuleni.

Amesema pia wameandaa mafunzo ya muda mfupi kwa walezi wa nyumbani ili waweze kupata elimu ya malezi kwa mtoto ambayo itasaidia kuwalea vyema.

“Kuna changamoto ya walezi wa watoto nyumbani kutojua umuhimu wa malezi bora kwa kumfokea mtoto au kumtishia hali inayosababisha kuwa na hofu ya kurudi nyumbani baada ya muda wa masomo kuisha,” amesema Kaino.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles