27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaanza kuwabana wanaopiga fedha za miradi

Na Esther Mnyika Mtanzania Digital

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Adolf Ndunguru kufuatilia mfumo wa mtandao wa wizi wa fedha za miradi unaohusisha maofisa wa wizara hiyo na wakurugenzi.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 23, jijini Dar es Salaam na Waziri huyo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba 24 ya mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji ya Tanzania(TACTIC) ambao utatekelezwa kwa miji 45 na utagharimu zaidi ya Sh trilioni moja uliohudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wabunge.

“Katika eneo la fedha za miradi kumekuwepo na changamoto hata kwa TAMISEMI, ninakuagiza mkalifuatilie mara moja, wakati mwingine fedha zinatumwa katika halmashauri na majiji,’’ amesema Mchengerwa.

Amesema baadhi ya Wakurugenzi wa majiji, miji na halmashauri na baadhi ya watendaji TAMISEMI, sasa lazima na sisi tujiangalie wanaoshirikiana na mtandao wa uwizi.

“Zinatumwa fedha takribani Sh milioni 500 kwa baadhi ya wakurugenzi zinatolewa fedha hizo na zote wanagawana, sasa hili ulifuatilie kwa sababu ninazo taarifa na ushahidi wa baadhi ya halmashauri tano ambazo wanaingiziwa fedha na zinatolewa kinyemela kisha kugawana,” amesema Mchengerwa.

Aidha amemuomba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni kuingilia kati suala hilo ili wanaohusika wote mfumo wa mtandao wa wizi wa pesa za serikali wachukuliwe hatua.

“Ninyi Wakurugenzi mmekasimiwa madaraka na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baadhi katika maeneo yenu zimepelekwa fedha za miradi na wengine hadi muda huu hazijaanza kutekeleza miradi husika, sasa usimamizi wa miradi hii, Katibu Mkuu isipokwenda vizuri sitajali ni nani amewekwa pale, nitamsimamisha kazi, nendeni mkachape kazi kuwasaidia Watanzania,” amesema.

Amesem Mkurugenzi ambaye ni mzembe anayeendekeza vitendo vya rushwa hatakuwa sehemu ya serikali inayoendeshwa na Rais Dk. Samia kwani katika kipindi chake hatakubali uzembe huo na hatakuwa na huruma zaidi ya kuchukua hatua.

“Mikataba tuliyoisaini imegharimu takribani dola za kimarekani milioni 410 zaidi yash. trilioni moja na utatekelezwa katika miji 45 na kwa awamu ya kwanza litajumuisha miji 12 ambayo ni jiji la Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Ilemela, Morogoro, Kahama, Kigoma Ujiji, Songea, Sumbawanga, Tabora na Geita,” amesema.

Waziri Mchengerwa amewataka wakandarasi waliopewa zabuni ya kujenga miradi wafanye kazi hiyo kwa weledi na wakati uliopangwa kwa mujibu wa mkataba huku akiwataka pia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi hiyo.

Naye Mratibu wa Miradi ya Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, Mhandisi Hamphrey Kanyenye amasema utekelezaji wa maeneo hayo 12 utaanza katika mwaka huu wa fedha na mradi utagharimu kiasi cha Sh bilioni 276.18 ikihusisha gharama za usimamizi ambazo ni Sh bilioni 17.05.

“Katika mikataba hiyo wanatarajia kujenga barabara zenye uzefu wa kilometa 147.54 kwa kiwango cha lami, madaraja, vivuko maji, taa za barabarani zenye mfumo wa kutumia umeme wa jua, njia za watembea kwa miguu ,mitaro maji ya mvua,masoko na bustani hivyo aliwata wakurugenzi kukamilisha miradi hiyo kwa muda ulipangwa.

Ameeleza kuwa wameanza kwa miji hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu, awamu ya pili itahusisha miji ya Babati, Bariadi, Bukoba, Iringa Kibaha, Korogwe, Lindi, Moshi, Mpanda, Mtwara, Musoma, Njombe, Singida, Shinyanga na Tanga huku awamu ya tatu ikiwa ni Bagamoyo, Bunda, Chato, Handeni, Ifakara, Kasulu, Kondoa, Mafinga, Makambako, Masasi, Mbinga, Mbulu, Nanyamba, Tunduma,Newala, Nzega, Vwawa na Tarime.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles