Na Anna Ruhasha , Sengerema
Serikali imeahaidi kutoa Sh million 400 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya Mama na Mtoto katika kituo cha afya Kamanga kilichopo wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumamosi Agosti 14, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake wilayani humo.
Awali, Mganga mfawidhi katika kituo hicho, Dk. Godfrey Silayo alisema kituo kinapokea akina mama wengi wajawazito ambapo kwa mwezi hulaza kina mama 40 hadi 50 na wagonjwa wengi ni 60 hadi 100.
Ameongeza kuwa kuna upungufu wa vitanda vya wagonjwa pamoja jengo la upasuaji hali inayopelekea wagonjwa wawili kulala kitanda kimoja na wenye uhitaji wa huduma kupewa rufaa katika Hospitali teule ya wilaya ya Sengerema ambayo iko umbali wa kilometa zaidi 30.
Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amemhakikishia waziri kuwa fedha za ujenzi wa wodi zikifika zitasimamiwa vizuri ili kuondoa changamo hiyo. Kituo cha afya Kamaga kinahudumia kata tatu za Nyamatongo, Kahumolo na Ngoma.