30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI UGANDA YASHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI MATAPELI KUPORA ARDHI

Grace Asio akiwa na mwandishi wa makala, Sidi Mgumia.
Grace Asio akiwa na mwandishi wa makala, Sidi Mgumia.

Na Sidi Mgumia- Osukuru, Uganda

ARDHI ya nchi zilizopo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ni mali kutokana kuwa na madini mengi na hivyo inagombewa na kuvamiwa na matapeli, waliojificha kwenye koti la uwekezaji.

Wananchi wengi wa Uganda hasa wale wanaoishi mikoani, wameanza kuliona joto la wawekezaji hawa matapeli.

Waathirika wakubwa ni wakazi waishio kwenye ardhi zenye utajiri hasa wa madini. Mbali ya kukutana na adha ya kutapeliwa, lakini pia husababishiwa uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuharibiwa vyanzo vyao vya maji.

Kitendo cha ardhi yao kuwa na mali, kimekuwa ni adhabu kwao, wanageuzwa watumwa, manamba na wako kwenye nchi yao, wanatapeliwa kirahisi kwa kuuza ardhi yao kwa bei ndogo na wengine kuitoa kwa kunyweshwa chupa kadhaa za pombe.

Pombe inapokuja kuwatoka, wanakuwa wameshasaini hati za mauziano na pale wanapothubutu kuuliza, kinachowakumba ni vitisho na kejeli kutoka kwa wanaojiita wawekezaji.

Mfano dhahiri wa hili ni mradi wa madini wa Sukulu Phosphate uliopo Osukuru nchini Uganda, ambao waendeshaji wakuu ni wawekezaji kutoka China chini ya kampuni ya Nishati ya Guangzhou Dongsong Energy Ltd, (GDE) Ltd.

Kampuni hiyo imepewa maeneo na Serikali katika kaunti za Osukuru na Rubongi katika Wilaya ya Tororo nchini Uganda.

Hata hivyo, wanakijiji wa eneo hilo wamekuwa wakilalamika kuondolewa katika maeneo yao kupisha uwekezaji huo kwa kupewa ahadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia ya maeneo yao.

Bahati mbaya hakuna fidia waliyolipwa na kinachowaumiza zaidi ni namna hila  na gilba ilivyotumika katika kusaini baadhi ya nyaraka za malipo.

Kutokana na kutokujua kusoma na kuandika kumewafanya wengi wao kusalimisha ardhi zao kwa kampuni ya (GDE) Ltd kwa kipindi cha miaka 99. Yale ya Mjerumani Karl Peters na Chifu Mangungu wa Msovero miaka 200 iliyopita nchini Tanzania yamejirudia nchini Uganda miaka hii.

Tayari ardhi imetwaliwa kwa ajili ya kufanya uchimbaji wa Phosphate katika Kijiji cha Osukuru, lakini bado wamiliki halali wa ardhi hiyo hawajalipwa fidia licha ya Serikali kuahidi kutekeleza jukumu hilo mara kadhaa bila mafanikio. Inasikitisha kuona Serikali inashirikiana na matapeli hao kudhulumu wananchi.

Sasa wanakijiji wamekuwa wakitaabika baada ya kukosa sehemu ya kilimo, walielekeza mategemeo yao kwenye kulipwa fidia zao, huko nako wamepoteza. Maisha yamekuwa magumu kwao wakati hakuna mahali pakukimbilia.

Hayo yalifahamika baada ya waandishi wa habari kutoka Tanzania na Uganda kutembelea eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mafunzo na uelewa juu ya masuala ya uchimbaji madini, mafuta na gesi waliyokuwa wakishiriki chini ya Taasisi ya kusimamia Rasilimali Asilia (NRGI) iliyoshirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), African Centre for Media Excellence (ACME)- Uganda na Penplusbytes ya Ghana.

Kwa mujibu wa wanakijiji 124, hadi sasa hakuna mwathiriwa hata mmoja ambaye amelipwa na wale waliolipwa wamelipwa fedha kidogo tofauti na viwango vilivyowekwa na Wilaya ya Tororo.

John Ayoro, mkazi wa Kijiji cha Aburirubongi, ni mmoja wa watapeliwa, aliwaambia waandishi kuwa utata uliopo kuhusu ni nani wanaofaa kulipwa fidia huenda ukachelewesha malipo hayo.

Ayoro aliilaumu Serikali Kuu kwa kile alichokitaja kuwa kuhusisha watu wachache katika suala hilo hali inayoleta ugumu.

“Ni heri wangefuata makubaliano ya awali kati ya waathiriwa na Serikali kufidia watu tuliotoa maeneo yetu kwa hiyari kwakuwa tuliahidiwa mambo makubwa yakiwemo maisha bora yenye utajiri mkubwa,” alisema Ayoro.

Aliongeza kuwa suala la kuwahusisha viongozi wa siasa analipinga na kuwa ni tatizo kubwa kwani hao ndio wanaochelewesha fidia zao ili na wao wapate.

Matukio kama haya ambayo yapo si Uganda tu bali hata hapa Tanzania na kwingineko, yamekuwa yakileta mitafaruku mikubwa baina ya wazawa na wawekezaji hali inayowasababishia kuingia kwenye mgogoro.

Hali kama hizi husababishwa na kutokuwekwa wazi kwa masuala yote muhimu yanayohusiana na aina ya uwekezaji na badala yake mambo yanaendehswa kwa upana baina ya Serikali na wawekezaji huku wanakijiji ambao ndio wahusika wakuu kushirikishwa kidogo sana hasa kwenye kuidhinisha kutolewa kwa ardhi.

“Serikali na wawekezaji walitufuata na kutushawishi kuachia ardhi zetu kwa madai kuwa watatulipa fidia halali kulingana na ukubwa wa maeneo yetu na kwamba mwekezaji atayachukua kwa miaka 21 tu nasi tutakuwa matajiri,” alisema Ayoro.

Tatizo kubwa linalomuwia vigumu Ayoro kulipigania eneo lake ambalo liko katikati ya eneo kubwa la uchimbaji huo wa madini ya Fosfeti  ni hati ya kiwanja, ambacho waliahidiwa kupewa mara tu baada ya kutoa maeneo yao.

Hadi sasa, kazi ya kuipigania haki yake imemgharimu, kwani Ayoro amefikia hatua ya kutaka kuchomewa nyumba yake huku akipewa vitisho vikali.

Rose Tibita, ambaye anamiliki sehemu ya ardhi iliyotwaliwa anasema, “Viongozi walikuwa wanakuja na kutuambia  tutalipwa milioni 49 au 30 kwa mwaka kwa muda wa miaka 21, jambo ambalo lilionekana jema kwetu sote na tukakubali kusaini mkataba na kutoa maeneo yetu tukiamini tutapa pesa nyingi kama tulivyoaminishwa,”.

Aliongeza kuwa kwa bahati mbaya sana hawajui kusoma na kuandika hivyo walisainishwa mikataba ambayo haikuandikwa walichoambiwa ikiwa na maana ya kwamba mikataba ilieleza kuwa ardhi itakuwa chini ya mwekezaji kwa miaka 99 na si 21 na hakuwepo na kipengele cha malipo ya mamilioni yale waliyotajiwa awali na kwa wachache wao walisalia kupata Ush 500,000 ambayo ni sawa na Sh 300,000 za Tanzania, kiasi ambacho ni kidogo kulinganisha na mahitaji yao na hasa ukizingatia wameshanyang’anywa ardhi ambayo ndio rasilimali wamekuwa wakiitegemea kujiingizia vipato kupitia kilimo na ufugaji.

“Hizi zote ni njama za Serikali kutulaghai kwani mwekezaji hawezi kutoka anakotoka na kuja kufanya mambo kiholela hivi. Serikali inahusika, tena pakubwa,” alisisitiza Tabita

Aliongeza kuwa, “Tulikatwa Ush. 120,000 (sawa na Sh 73,285 za Tanzania), ili tupatiwe hati za ardhi lakini mpaka leo hatujapata. Kwa ujumla wawekezaji hawajafanya maendeleo na mabadiliko yoyote na badala yake maisha ndiyo yamezidi kuwa magumu. Lakini pia bado mradi hauwapi fursa za ajira wazawa wa eneo letu, wanaajiriwa watu kutoka maeneo ya jirani na hata nje ya Uganda.”

Ilielezwa kuwa, ulipaji huo wa fidia umekwama kutokana na mwekezaji huyo kutotaka kulipa fidia yote kwa wakati mmoja bali anataka alipe fidia kidogo kwa kuanzia na eneo dogo kati ya lile analomiliki ambalo anadai ndilo atakaloanza kufanyia kazi.

Aidha, alidai kwamba atakuwa analipa fidia kwa eneo lililobaki kulingana na atakavyokuwa akilitumia.

Na pia wanalalamika kwakuwa mwekezaji hataki kuzungumza na wananchi husika ili wakubaliane kiasi cha fidia atakachotoa kwao kwa kuzuia shughuli zao za kujipatia kipato katika eneo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Kwa upande wake Aruso Nyango, anasema yeye anapenda wawekezaji lakini haoni faida yao kwakuwa wameendelea kuwa masikini.

“Mimi nililazimishwa hadi kufukua maiti zilizokuwapo katika eneo langu na kuwa nitalipwa milioni 1 na badala yake nikalipwa 500,000 tu,” alisema Nyango.

Kwa upande mwingine, Jattawa Awengi, anasema japo bado hajalipwa fidia, haruhusiwi hata kunywesha mifugo yake maji katika eneo lake ambalo bado halijafikiwa kwa uchimbaji huo kwa madai kuwa kwasasa ni mali ya mwekezaji.

“Tumekuwa tukitishiwa na majeshi pale tulipojaribu kudai stahili zetu, kwakweli tunaishi maisha ya woga sana katika nchi yetu hii, tunataabika sana,” aliongea Awengi kwa huzuni.

Akiongelea suala hilo la changamoto za wawekezaji, Grace Asio ambaye ni mwenyekiti wa Kijiji cha Aburiye, alisema wawekezaji hao katika kijiji chao hawajaweza kutoa mchango wowote kwa jamii kwani pamoja na uwepo wao bado wanategemea chanzo kimoja cha maji, kituo cha afya kimoja na kisichotosheleza mahitaji yao pia kipo umbali wa kilomita 5 kutoka kijijini.

“Na tunashangazwa sana na Serikali kwani inayatambua  madhila yote haya yanayotukumba lakini haifanyi chochote na hapo tunapata jibu kuwa inawafurahia wawekezaji kuliko sisi wazawa,” alisema Asio.

Asio alisema kuchukuliwa kwa ardhi za wanakijiji hao kutoka katika kaya 213, kumewaletea balaa kubwa na sasa wana njaa kali, watoto wa kike wanapata mimba ovyo kwakuwa wanatafuta namna yakujisaidia kimaisha, wanajifungulia nyumbani kwakukosa miundombinu.

“Serikali imekuwa ikija kila mara kupima maeneo yetu na baada ya hapo wanaondoka bila kutuachia hata mawasiliano yao na pia wanavyoviandika kwenye makabrasha yao huondoka navyo pasi wananchi kujua wameandika nini na kuachwa na sintofahamu ya nini itakuwa hatima yao,” alisema Asio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles