Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesisitiza marufuku yake aliyoitoa hivi karibuni kuhusu ajira kwa watoto ambao wapo chini ya miaka 18.
Mhe Hasunga amepiga marufuku hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusuala la ajira kwa watoto ni miongoni mwa mambo yanazuiliwa kwenye sheria za kimataifa kupitia Shirika la Kazi Duniani (International Labour Organization) na Sheria za Ajira hapa nchini hivyo mdau yeyote atakayebainika kukiukwa maelekezo hayo atashtakiwa.
“Nawasihi wadau wote hususani wakulima wa tumbaku tuendelee kupiga vita ajira kwa watoto kwa kuwa ni eneo ambalo limeendelea kulalamikiwa na wadau wengi,” alisema Hasunga
Hata hivyo alisema kuwa katika kuhakikisha zao la tumbaku linaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la mkulima na Taifa, Wizara imejiwekea malengo ya haraka yanayopaswa kutekelezwa ambayo ni pamoja na usajili wa wakulima wote wa tumbaku.
“…kuwapatia vitambulisho na kuwaingiza kwenye kanzidata ili kupata takwimu za uhakika za maeneo wanayolima na kuiwezesha serikali kusimamia upatikanaji wa pembejeo kulingana na mahitaji yao,” alisema
Ailiitaja mipango mingine ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati kwa kuweka utaratibu wa kumwezesha mkulima kujitegemea kwa pembejeo ili aache kuwa tegemezi wa mikopo ya mabenki yenye riba kubwa.
Pamoja na malengo hayo ya haraka, Wizara ya Kilimo inasimamia utekelezaji wa malengo ya muda mrefu yakiwemo Upatikanaji wa wanunuzi wapya wa tumbaku kwa sasa na kwa miaka ijayo kabla ya Juni, 2020, Kuongeza ubora wa zao la tumbaku kutoka asilimia 87 ya sasa hadi asilimia 92 ifikapo Juni 2022 na kuongeza mbegu mpya na bora za tumbaku ili tuweze kupata masoko katika nchi nyingine kama vile China.
Alisema ili kufikia malengo hayo wadau wote wa tasnia ya tumbaku wanapaswa kushirikiana ili kufikia malengo hayo na wakulima kunufaika na jasho lao.
Tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu ya kimkakati ya yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli ambapo mazao mengine ni pamoja na Tumbaku, Kahawa, Pamba, Korosho, Chai, michikichi na alizeti.