31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuboresha sera ya miliki bunifu

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Serikali imeweka wazi kuwa inaendelea kuboresha sheria na sera ya miliki bunifu ili kuhakikisha  yanakuwepo mazingira rafiki yenye tija kwa wabunifu na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘ Mwana FA’ wakati alipomuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji katika maadhimisho ya siku ya Miliki Bunifu duniani yalifanyika leo Mei 9,2024, jijini Dar es Salaam.

Mwana FA amesema ubunifu ni nyenzo muhimu katika kukuza na kuendeleza biashara, uboreshaji wa sera utaondoa changamoto na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja nchini.

“Wizara ya viwanda na biashara imekuwa ikitoa muongozo kwa BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni), kufanya kazi na taasisi nyingine zinazosimamia au kuratibu masuala ya ubunifu ili kuweka mazingira rafiki kwa wabunifu,” amesema Mwana FA.

Aidha ameilekeza BRELA kuwatambua wabunifu na kuhakikisha wanapata dhamana zinazowawezesha kukopesheka kwa ajili ya kuendeleza kazi zao.

Pia ameipongeza BRELA kutokana na kazi wanayoifanya hasa katika kuwafanya   wafanyabiashara na wenye makampuni kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema wanashirikiana na taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ni bora na kuondoa migogoro.

Ameeleza kuwa uelewa wa miliki bunifu hapa nchini bado upo chini, hivyo wanaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuongeza idadi ya wabobezi watakaoisaidia jamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Viwanda(UNIDO), Vedastus Timothy ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira yanayoendelea kuboresha na kuchochea ubunifu.

Katika maadhimisho hayo BRELA imesaini hati za makubaliano ya ushirikiano na taasisi nne tofauti ili kushirikiana kutoa ushauri na mafunzo kwa watafiti na wajasiriamali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles