25.9 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI ISIRUDIE MAKOSA MIKATABA ISIYO NA TIJA

BUNGE limepitisha sheria ya kuivunja Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) iliyokuwa ikimilikiwa kwa mujibu wa sheria na Kampuni ya RITES ya India.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mpya iliyopitishwa juzi, Shirika Hodhi la Mali za Reli (RAHCO) nalo pia limevunjwa na kuundwa Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Uamuzi huo, ulipitishwa chini ya sheria ya mwaka 2017, baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Reli ya mwaka 2017.

Katika muswada huo, Profesa Mbarawa alisema wakati TRL ikimilikiwa kwa ubia na RITES, Serikali ilikuwa ikimiliki asilimia 49 na kamuni hiyo ya India ilikuwa ikimiliki asilimia 51.

Alisema wakati wa ubia huo, TRL ilikuwa haijiendeshi vizuri na uendeshaji huo mbovu ndio uliosababisha Serikali kuirudisha TRC kwa kuwa ilikuwa ikijiendesha kwa faida.

Wote tunaamini kabla ya kuja TRL, tulikuwa na TRC ambayo ilikuwa imara na iliweza kufanya kazi zake kwa uhakika bila ubabaishaji.

Tunakumbuka kuwa TRC ilikuwa mali ya Serikali kabla ya kuingia ubia na RITES kutokana na sababu mbalimbali na kuundwa TRL.

Wakati wa uendeshaji wa TRL chini ya wabia RITES, tulishuhudia madudu mengi.

Ni ukweli kuwa tangu RITES kuingia ubia, TRL haikujiendesha vizuri, tulishuhudia migogoro mingi  kati ya menejimenti na wafanyakazi kila kukicha na kuwapo mikataba mingi isiyokuwa na tija.

Tunaungana na uamuzi wa Serikali kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Reli ya mwaka 2017 uliovunja TRL na RAHCO ambazo hazikuleta matunda yaliyotarajiwa.

Tumelazimika kuyasema haya kutokana na ukweli kuwa mikataba mibovu imekuwa ni janga kwa taifa kwa miaka mingi sasa.

Tunaamini kuwa kuvunjwa kwa TRL na kuirejesha TRC chini ya mikono ya Serikali, kutaleta tija kwa shirika hilo, Watanzania na taifa kwa ujumla.

Tunaamini sasa TRC itajiendesha kwa faida kutokana na namna wizara husika itakavyojipanga.

Ni ukweli usiopingika kwamba kuwapo mgawanyiko kati ya TRL na RAHCO, kulisababisha kushusha  utendaji kazi.

Tunaamini kurudishwa kwa TRC kutaongeza ufanisi na utendaji kazi mara dufu, hatutasikia tena “leo treni haitafanya safari” na mamia ya abiria kukwama stesheni kwa sababu ambazo wakati mwingine hazina msingi.

Tunasema hivyo kwa sababu, tumeshuhudia mara kadhaa abiria wakitaabika, wengine wakilazimika kuhamishia makazi katika vituo vya treni kutokana na kutokuwapo usafiri licha ya kuwa tayari walishakata tiketi.

Ili kuepusha makosa yaliyokuwa yakifanyika huko nyuma, Serikali sasa iwe na utaratibu mzuri kwa abiria kupata haki zao pindi inapotokea safari kuahirishwa kwa sababu mbalimbali.

Kwa kufanya hivyo, kutaonyesha wazi namna ambavyo shirika linawajali wateja wake kwa sababu usafiri wa treni ni kimbilio la Watanzania wengi.

Hatuamini kama TRC mpya inayokuja, itarudia makosa ya TRL katika utendaji kazi.

Tunawasisitiza watendaji watakaokabidhiwa majukumu watimize wajibu wao kwa masilahi mapana ya taifa ili kufikia malengo.

Tunamalizia kwa kumpongeza Profesa Mbarawa kwa uamuzi aliochukua kuivunja TRL na kuirejesha TRC na ndiyo maana tunaishauri Serikali isirudie makosa ya mikataba isiyokuwa na tija.

Pia tunaisihi Serikali kuhakikisha watumishi wote waliokuwa wakiyafanyia kazi mashirika hayo kabla kuvunjwa wanalipwa stahili zao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles