30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

“Serikali imepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU na UKIMWI nchini”-Mhagama

*Kiwango cha upimaji VVU chaongezeka kutoka 61% hadi 83%

*Vifo vitokanavyo na VVU vyapungua kwa 50%

*Rais Samia Suluhu mgeni rasmi siku ya UKIMWI Mbeya

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mujibu wa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 hadi asilimia 83 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU).

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Jumapili Novemba 14, jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2021.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kasper Mmuya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko (kulia) wakati mkutano huo uliofanyika Novemba 14, 2021 katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama ameeleza kuwa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilima 61 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

“Serikali kupitia uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” amesema Waziri Mhagama.

Amefafanua kuwa, matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka 95% mwaka 2016 hadi 98% mwaka 2019 na Kiwango cha kufubaza VVU kwa wale wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka 87% mwaka 2016 hadi 92% mwaka 2019.

Pia amebainisha kuwa vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa 50% kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.wakati takwimu za kiwango cha maambukizi katika jamii (HIV prevalence) zinaonyesha kiwango kilishuka kutoka 7% mwaka 2003/04 hadi 4.7% manamo mwaka 2016/17.  

Sehemu ya washiriki kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), UNAIDS na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOFA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.

Mhagama amefafanua kuwa Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) nchini Tanzania yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020. Wakati Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Mother to child transmission) yameshuka kutoka 18% mwaka 2010 hadi 7% mwaka 2020.

Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu 2021 amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kitaifa Jijini Mbeya kuanzia Novemba 24 hadi Disemba 1, 2021 katika Uwanja wa Luanda Nzovwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan yakiwa na kauli mbiu ya “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutoa fursa ya kutathimini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi va UKIMWI (VVU) na UKIMWI kitaifa na kimataia, kutafakari na kutekeleza kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana vipaumbele vya kidunia kwa muktadha wa kitaifa, pamoja na kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI.

“Katika wiki ya maadhimisho hayo kutakuwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF) ambayo yatafanyika Novemba 24, 2021 jijini Mbeya. Pia kutakuwa na kongamano la kisayansi kwa ajili ya kutathmini hali na mwelekeo wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” amesema Waziri Mhagama.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa kutakuwa na Kongamano ambalo litahusisha mawasilisho ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini.

Chuo cha MUST Mbeya.

Pia kutakuwa na mdahalo wa vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vilivyopo Mkoani Mbeya ambapo watajadiliana masuala mbalimbali yanayo husiana na afua za VVU na UKIMWI kwa vijana, mafanikio yaliyofikiwa vyuoni katika kukabiliana na changamoto hizo. Pamoja na hayo ameongeza kuwa kutakuwa na Mdahalo wa Viongozi wa Dini na Viongozi wa Jadi (Machifu), utakaohudhuriwa na vijana na jamii kwa ujumla

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza Wakuu wa Mikoa  yote nchini kusimamia utekelezaji wa shughuli za maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani katika mikoa yao kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI walioko katika Mikoa husika.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wakazi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani watumie fursa ya maonesha hayo kupata elimu ya afya,ushauri nasaha,upimaji wa hiari wa VVU, Upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi, Sukari, Uwiano wa Urefu na Uzito wa Mwili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko aliishukuru Serikali kwa kuendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Sehemu ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, jijini Dodoma.

Naye Mwenyekiti wa Baaza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Leticia Kapela ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita namna inavyoendelea kuwajali watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na mikakati iliyojiwekea katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambayo yameleta mafanikio makubwa na maambukizi kupungua.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi watu tunaoishi na virusi vya UKIMWI na sisi Baraza tutahakikisha tunashirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,” amesema Kapela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles