Na Mwandishi wetu
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imewataka wazazi na jamaa wa wanafunzi 420 walioko Jimbo la Hubei katika mji wa Wuhan nchini China, ambao ndio kitovu cha maambukizi ya virusi vya homa ya corona (Covid-19) kuwa watulivu na kwamba Serikali haitawarudisha nchini kwa sababu kuna karantini iliyowekwa kwenye mji huo.
Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano, Emmanuel Buhohela ilisema hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyepo China ambaye amebainika kuambukizwa virusi hivyo na hivyo kuwasihi wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia hali zao kwa karibu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao kwa kuwa wako katika uangalizi maalumu nchini humo.
Ilisema uamuzi huo unatokana na Serikali kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji wa Wuhan kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo.
“Uamuzi wa Serikali kutowaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao kurejea nyumbani, unatokana na taarifa za kitabibu zinazobainisha kutokea milipuko ya homa ya virusi hivyo katika mataifa ambayo awali yaliwaondoa wananchi wao wakati wa mlipuko na kusababisha kusambaa kwa virusi hivyo na kuleta madhara zaidi kwa mataifa hayo.
“Serikali inawasihi wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi hao kuwa watulivu na kuepuka kutumika kisiasa katika suala hili la virusi vya corona, kwani magonjwa hayana siasa na virusi hivi ni hatari kwa mtu yeyote na vinasambaa kwa kasi.
“Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake uliopo Beijing, imeendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na ofisi za kimataifa za vyuo vikuu walipo wanafunzi kutoka Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwapatia vifaa vya kinga ikiwamo viziba pua (masks) na sabuni maalumu za kunawa mikono (disinfecants) pamoja na kusaidia utatuzi wa mahitaji ya lazima pale inapojitokeza,” ilisema.
Taarifa hiyo ilisema tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amewasiliana kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi kuhusu hali za Watanzania na amemuhakikishia usalama wao.
Kwamba pia Serikali inakamilisha mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia za simu (hotline) zitakazotumiwa na wataalamu wa saikolojia (psycho-social support) kuwapatia ushauri nasaha wanafunzi na wazazi wakati juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea.
Kuanzia Januari, mwaka huu, China ilikumbwa na mlipuko wa homa ya corona (the novel coronavirus- 2019-nCoV) ambavyo jina lake rasmi kwa sasa kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni Covid–19.