29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI: DK. SHEIN HAFANYI KAZI KWA SHINIKIZO

 

Na BAKARI KIMWANGA-ZANZIBAR

 

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema suala la uwapo wa mabadiliko ndani ya Serikali linalofanywa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, lipo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na si shinikizo la mtu kama inavyodaiwa.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja baada ya kuibuka kwa madai kwamba ujumbe wa Sultani Qaboos bin Said wa Omani aliyetuma meli yake ya kifahari iliyobeba ujumbe wa amani kwa nchi za Afrika Mashariki, uliibana Serikali ya Dk. Shein kuhusu hali ya kisiasa.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa SMZ, Issa Haji Gavu, alisema si kweli kwamba Dk. Shein alibanwa na ujumbe huo kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi na ule wa marudio uliofanyika Machi, mwaka jana.

 

Gavu alisema ujumbe wa Sultan Qaboos ulikuwa na lengo maalumu la kuimarisha ushirikiano na si masuala ya kisiasa Zanzibar.

 

“Ninapenda kujibu suala hili kuwa katika ujumbe ule hakuna sehemu yoyote si rais au kiongozi mwingine wa Serikali aliyeulizwa kuhusu masuala ya ndani ya Zanzibar, Dk. Shein hajabanwa kama wanavyovumisha wanasiasa wengine.

 

“Unapomalizika uchaguzi, kazi ya Serikali yoyote iliyopewa ridhaa huwa ni kuwahudumia wananchi kwa ajili ya maendeleo na wale waliokosa ni kazi yao hubaki kusema, hivyo nasi kama Serikali hatuwezi kuwaziba midomo.

 

“Sasa eti wanavumisha Rais Dk. Shein amebanwa na ujumbe wa Sultani, hili si kweli jamani ni uvumi uliokuwa kabla na utaendelea kuwepo,” alisema.

 

Alipoulizwa kuhusu mabadiliko ya Dk. Shein kwa makatibu wakuu wa wizara mbalimbali aliyofanya hivi karibuni kuwa ni moja ya mkakati wa kurudi kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama inavyodaiwa na CUF, Gavu, alisema suala la mabadiliko lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kumpangia rais pindi anapotimiza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

 

“Ninataka kuwaambia hao wanaopita na kusema kuwa mabadiliko haya kuna Serikali ya Umoja, hakuna jambo kama hilo, wananchi walishaamua na sasa Serikali inafanya kazi. Na wale ambao kila siku kazi yao ni kusema tu wasome Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 wajue majukumu ya Rais wa Zanzibar na si kuendelea na uvumi wa mitaani,” alisema.

 

Kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na ujumbe wa Sultani Qaboos, alisema Zanzibar imefanikiwa katika uwekezaji, utalii na ajira kwa vijana zitakuzwa.

 

“Oman na Zanzibar zina udugu wa kidamu kutokana na asili yake, sasa Zanzibar itanufaika, Serikali ya Oman imekubali kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha samaki na matunda na si hilo tu pia kwa sekta ya utalii napo tumejadiliana namna watalii kutoka Oman watakavyokuja hapa nchini ikiwamo kuongeza safari za ndege,” alisema.

 

Kwa upande wake, Mshauri wa Rais wa Zanzibar Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia, alisema Zanzibar imefanikiwa kukuza uhusiano na nchi mbalimbali ikiwemo Oman na kwa sasa kuna mafanikio mengi.

 

“Kuna watu wanasema kwanini Dk. Shein hafanyi ziara nje ya nchi, ninataka kusema hapa tupo vizuri sana katika masuala ya diplomasia, kwa mwaka huu peke yake amepokea ujumbe kutoka kwa mabalozi mbalimbali ambao nchi zao zinataka ushirikiano na Zanzibar,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles