Na MALIMA LUBASHA – SERENGETI
ZAIDI ya tani 4.1 za chakula zinahitajika wilayani ya Serengeti mkoani Mara ili kunusuru maisha ya kaya zaidi ya 32,000 kutokana na mahindi yao kukauka kutokana na ukame.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alisema hali ya chakula kwa mwaka huu sio ya kuridhisha kutokana na mvua vuli kutonyesha kwa wakati.
Alisema wapo baadhi ya watu, wanakula mlo mmoja na wengine mitatu kwa siku na hakuna mtu wala mifugo iliyokufa kutokana na ukame, kwa sasa bei ya mahindi debe moja linauzwa Sh 15,000 ambapo upatikanaji wa chakula kwenye masoko wa kiwango kinachohitajika.
Alisema wilaya bado inaendelea kufanya tathimini kwa kupita kila kaya ili kubaini hali ya chakula kwa wale wenye upungufu wa chakula, kaya zisizo na uwezo,zenye uwezo na zile zinazohitaji msaada wa chakula na tayari wameomba kibali ili wafanyabiashara waruhusiwe kuuza mahindi kwa bei nafuu.
“Maofisa kilimo wamefanya tathimini kwenye kaya 32,055 zilizopo katika kata 22 kati ya 30,wamebaini kaya 8,582 ambazo ni maskini zinahitaji chakula cha bure tani 811, kaya 10,655 wenye hali ya nafuu wanahitaji tani 1,454.4 na kaya 12,818 zilizo na uwezo wa kununua kwa bei yoyote zinahitaji tani 1,749.7 za mahindi,” alisema Babu.
Hata hivyo, Babu amewataka wananchi kuhifadhi chakula kilichopatikana na kuacha utamaduni wa kutumia nafaka kutengenezea pombe za kienyeji na kila familia iwe na ghala la kuhifadhi chakula.
Alisema mbali ukame, mvua kutonyesha kutokana na mabadiliko ya tabianchi pia yapo malalamiko ya wananchi kuhusu tembo kuvamia mashamba yao na kula mazao yote na kueleza kuwa changamoto hiyo serikali inalifahamu na takwimu za uharibifu zilikwisha wasilishwa wizara ya maliasili na utalii ili kuli pa kifuta machozi kwa wote walioathirika.