29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sera mpya za Chadema ni ushindani si upinzani

Na EVANS MAGEGE

Wapo baadhi ya watu kwa hulka zao wanaweza kupuuza ama kubeza sera mpya za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kuwa zimetolewa na chama cha upinzani.

Sera hiyo mpya inaonekana katika sura ya kushindana na si upinzani wa kisiasa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama tawala nchini.

Mtu mwenye tabia ya kusoma mambo na kufikiri sawasawa anaweza kuwa na mtazamo tofauti kabisa na watu wa kaliba hiyo niliyoieleza hapo juu.

Yamkini baadhi ya watu kutoka chama tawala wanawaona Chadema si wapinzani tu bali ni mapepo wabaya(adui), kwa mtu aliye huru kifikra, namaanisha mtu ambaye akili yake haijasongwa na itikadi za vyama vya siasa, katika hoja hizo 12 za Chadema, ataziona baadhi kuwa ni hoja bora na zenye masilahi mapana ya nchi yetu.

Kutokana na muktadha huo msingi wa makala haya unapoanzia.

Kwanza kabisa Chadema wanaamini kuwa Sera hiyo ni mahususi katika kujipambanua kwa umma kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Katika mtazamo mpana wa kifikra ni jambo jema kwa chama cha siasa kuwa na sera zenye kuufikirisha umma, lakini ni vema zaidi kwa Chadema kufanya hivyo kwa kuwa ndicho chama kikuu cha upinzani nchini na hatua hiyo ni dalili nzuri ya ukomavu wa kisiasa ndani ya miaka 26 tangu kuzaliwa kwa chama hicho.

Hoja 12 zinazojenga sera hiyo mpya ya Chadema ni Utawala, Uchumi wa Soko Jamii, Siasa za Ndani, Siasa za Kijamii, Elimu na Sayansi, Afya, Uamuzi wa Ardhi, Kilimo, Miundombinu, Mazingira na Mambo ya Nje.

Kwa kiasi kidogo cha hoja za sera hiyo mpya nilizozisoma na kujifikirisha nimeuona mtazamo wa masafa marefu wa Chadema kuendelea kusimama katika medani za juu za siasa za nchi hii ingawa sikioni chama hicho kikijinasua kwenye kilevi cha kucheza ngoma zinazopigwa na CCM.

Jambo ambalo Chadema wanajitahidi kufanikiwa katika makuzi yake, ni kujitambua wao kama washindani wa CCM na si wapinzani wa CCM mtazamo ambao ni kinyume kabisa na wafuasi wengi wa CCM ambao wanaona Chadema ni chama pinzani kwao kama ilivyo kwa vyama vingine vilivyopo  katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Wafuasi hao wamekuwa wakiishi katika mtazamo huo kwa muda mrefu na wameendelea kutambua kuwa Chadema ni chama pinzani kama ilivyo UDP, CUF, NCCR –Mageuzi  na kadhalika na hawajipi nafasi ya kushtuka walau kidogo kuangalia historia za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 au 2010.

Hawajiulizi sababu ya Chadema kuweka sera zao wazi kwa umma na kwanini wanajiamini kufanya hivyo wakati vyama vingine vimeficha sera ndani.

CCM kama taasisi kongwe pamoja na uzoefu wake wa kutawala nchi, mfumo mzuri wa kujirekebisha pale wanapohisi waliteleza wanatambua vyema uwapo wa Chadema.

Ndiyo maana hata uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuweka katazo la mikutano ya vyama vya siasa majukwaani kwa ngazi ya kitaifa au maandamano ya kisiasa, badala yake hoja zipelekwe bungeni au wasubiri uchaguzi ujao bado haujafifisha hisia za umaarufu wa Chadema akilini mwa watu ingawa shughuli zake zimepotea machoni mwa watu.

Kwa mara kadhaa huwa najiuliza mazingira ambayo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposoma msimamo wa kisera wa Chadema wa mwaka 1993 na kukiri kuwa chama hicho ndicho kitakachofuata katika kuiongoza Tanzania. Je; alikuwa kanuna au akitabasamu, alikuwa anatania au anamaanisha kuwapo kwa siku isiyokuwa na jina kwamba anguko la CCM litatimia na Chadema wakatwaa hatamu.

Licha ya mwenendo huo wa Chadema pamoja na mapungufu au makosa mbalimbali iliyonayo, hata hivyo bado kinajengwa kwenye misingi imara pindi kinapochomekewa vihunzi mbalimbali vya kisiasa kama ilivyokuwa kwa NCCR-Mageuzi na CUF.

Katika hoja ya kwanza kati ya hoja 12 za Sera  Mpya za Chadema wamezungumzia suala la Katiba jambo ambalo nalizungumzia.

Hoja hiyo wameijenga kwa vipengele vinne ambavyo ni Haki za Binadamu, Uhuru Thabiti wa Kujieleza, Mfumo wa Utoaji wa Haki pamoja na Utawala wa Sheria.

Ufafanuzi wa ujumla wa hoja hiyo ambayo wameigawa katika vipengele vinne wanaeleza kwamba Katiba inayotokana na wananchi ni waraka ambao unajumuisha maoni na mapendekezo ya wananchi juu ya jinsi wanavyotaka kuongozwa katika nchi yao.

Kwamba Chadema wanaamini Katiba lazima itokane na maoni na mapendekezo ya wananchi juu ya namna wanavyotaka wajitawala na namna wanavyotaka dola pamoja na taasisi na mashirika mengine yaendeshwe.

Wanaamini kuwa Katiba itakuwa na uhalali pale tu matakwa ya wananchi yatakapoheshimiwa katika nyanja zote za maisha.

Hoja hiyo pia inaeleza kuwa Katiba inatarajiwa kuweka misingi na kutamka kinagaubaka juu ya mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu ya Dola na pia kuweka misingi ya kudhibitiana baina ya mihimili hiyo ili kulinda haki za binadamu.

Kimsingi hoja yao ya Katiba naiunga mkono kwa umuhimu wa dhana yenyewe kwa mahitaji ya Tanzania ya sasa lakini si sababu zote walizozianisha, ingawa uhalisia ni kwamba uhitaji wa Katiba Mpya au maboresho ya Katiba bado ni mkubwa kwa wananchi, lakini najizuia kuingilia maoni ya watu kwamba wanahitaji katiba ya aina gani.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete  na vyombo vyake waliliona hilo suala la uhitaji wa Katiba Mpya kwa wananchi ndiyo maana aliitisha mchakato ambao ulizalisha rasimu ya kwanza na ya pili  kumalizika kwa mpasuko mkubwa wa kisiasa ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa wanaeleza kuwa moja ya sababu ya Bunge hilo kupasuka kisiasa ni mtazamo wa wajumbe wenyewe ambao wale waliotokana na vyama vya siasa za upinzani kuitetea rasimu iliyowasilishwa na Tume  ya Katiba,  walihisi kuwa wajumbe  kutoka chama tawala (CCM) walihodhi  hatua hiyo ya mchakato kwa lengo la kuingiza mapendekezo yenye matakwa yao.

Hata hivyo upo mtazamo unaodai kuwa suala la Katiba Mpya halikuwa ajenda ya CCM hivyo uamuzi wa Rais Kikwete kuanzisha mchakato huo ulikuwa sawa na dhamira ya kujitumbua mwenyewe madarakani.

Ni wazi kuwa Chadema wameweka hoja hii ya Katiba kwa kuamini kuwa suala la uhitaji wa Katiba Mpya ndani ya nchi lipo mawazoni mwa watu, lina nguvu na linaendelea kuishi kwenye fikra  na vichwa vya Watanzania wengi, ingawa ipo mitazamo inayoliona suala hilo si pendwa ndani ya chama tawala na mifumo yake.

Kwa muktadha huo,  hoja hiyo ya Katiba inaweza kuendelea kushawishi polepole mifumo ya chama tawala labda ipo siku itaona umuhimu wa kuwapo mabadiliko, lakini lipo zingatio la kwamba ndani ya  kipindi cha kwanza cha Utawala wa Awamu ya Tano, suala la Katiba Mpya si kipaumbele.

Bado naendelea kuchambua na kuchambua zaidi ufafanuzi wa hoja hizo 12  ambazo Chadema wameziweka kama mhimili mkuu wa sera yao ya mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles