25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SAUT yazindua Kigoda cha Utafiti cha Mkapa

*Balozi Prof. Mahalu amtaja kuwa ndiye muasisi wa vyuo vikuu binafsi nchini

Na Clara Matimo, Mwanza

Chuo Kikuu  cha Mtakatifu Augustino(SAUT) kilichopo jijini Mwanza, jana Novemba 12, 2022, kilizindua Kigoda cha Utafiti cha Benjamin Mkapa ambacho  kitajikita zaidi kwenye tafiti na mafunzo lengo likiwa ni kuenzi mchango wake katika kukuza  sekta ya elimu ya juu nchini.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika chuoni hapo, Makamu  Mkuu wa Chuo  hicho, Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu, alisema SAUT ni matokeo ya Hayati Benjamin William Mkapa kwani  ndiye muasisi wa sera ya uanzishwaji wa vyuo vikuu binafsi nchini pamoja na  bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.  

“Mwaka 1992 utakubwakwa kuwa mwaka wa mapinduzi ya kisera, ni mwaka ambao mimi binafsi nakumbuka nikiwa Mkurugenzi wa Elimu ya juu na Hayati Mkapa alikuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, maono yake yalikuwa ni kuona vijana wengi wanapata elimu ya juu lakini changamoto ilikuwa ni uchache wa vyuo wakati huo tulikuwa na vyuo vikuu viwili tu hapa nchini.

“Alijitahidi sana kushawishi sekta binafsi kuwekeza kwenye utoaji wa elimu ya juu nchini wote mnakumbuka sekta binafsi ilivyokuwa imepoteza kujiamini kutokana na matokeo ya sera za utaifishaji lakini  kupitia Hayati Mkapa, serikali ilifanikiwa kuishawishi sekta binafsi na kuingia makubaliano ya kuwahakikishia usalama kwenye uwekezaji wao, matokeo yake ndiyo haya leo maelfu ya vijana wako vyuo vikuu binafsi kikiwemo SAUT kilichoanzishwa mwaka 1998 ikiwa  ni zao la iliyokuwa Taasisi ya Elimu ya Sayansi ya Jamii(NSTI),”alisema Balozi Prof. Mahalu.

Balozi Prof. Mahalu alieleza kwamba kabla ya mwaka 2005  serikali ilikuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya serikali peke yao hivyo vijana wengi wenye sifa ya kusoma vyuo vikuu walikosa fursa kutokana na wazazi au walezi wao kushindwa kumudu gharama lakini nia ya dhati ya Hayati Mkapa kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu ya juu iliendelea konekana na kudhihirika kwani mwaka 2005 kabla hayamaliza muda wake wa urais wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi nao walianza kupewa mikopo.

Makamu  Mkuu wa Chuo CHA SAUT, Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu, akiwa amekaa kwenye kigoda cha Utafiti cha Mkapa baada ya kuzinduliwa na Anna Mkapa.

“Hayati Mkapa alikuja hapa SAUT mwaka 2001 kwenye mahafali ya kwanza ya chuo hiki kama mgeni rasmi wakati huo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekuwa Makamu Mkuu wa SAUT wakati huo, Dk. Padri Deogratius Rweyongeza, aliiomba serikali kubadili sera ya mikopo kwa elimu ya juu ili ianze kuwapa mikopo na wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi, Hayati Mkapa aliahidi wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi wenye sifa wataanza  kupata mikopo kabla hajatoka madarakani, na kweli mwaka 2005 ombi hilo alilitekeleza wakati huo  SAUT ilikuwa na wanafunzi chini ya 400  sasa tuna wanafunzi zaidi ya 16,000, mafanikio hayo yametokana na mikopo inayotolewa na Serikali,”alisema Balozi Prof. Mahalu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema mambo mengi yanayopewa mkazo na kipaumbele kwenye serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni mwendelezo wa yale aliyoyayaanzisha Hayati Mkapa  ikiwemo bima ya afya ambayo sasa Serikali iko katika mchakato wa kuhakikisha kila Mtanzania anufaika nayo.

“Hayati Mkapa ameacha alama ambayo inagusa mioyo, macho na masikio ya vizazi vya sasa na vijavyo kwani alishika madaraka kukiwa na mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa lakini aliyatengenezea misingi na kuyasimamia maana aliamini katika utekelezaji wa uchumi wa ubia.

“Ni rais anayekumbukwa na wengi kwa kauli yake ya uwazi na ukweli, alifungua uchumi wa ushindani na siasa za ushindani, alitumia sekta binafsi kufikia malengo ya kijamaa,”alisema Malima.

Naibu Mkuu wa Skuli ya Sheria-Taaluma Zanzibar, Wakili Msomi, Msemo Mavare alisema  tasnia ya sheria itamkumbuka Hayati Mkapa kwa mchango wake katika utawala wa sheria kwani ndiye Rais mstaafu pekee Afrika aliyekwenda mahakamani kutoa ushahidi kumtetea Prof. Costa Ricky Mahalu wakati anashtakiwa alikuwa tayari kuhojiwana na wanasheria ili haki itendeke.

“Mimi  kila mara huwa nasema kwamba mtu mwenye uthubutu wa kuona haki inatendeka hata kama mbingu zitabomoka alikuwa ni Benjamnin William Mkapa, hakuwa mwanasheria lakini mchango wake katika tasnia ya sheria hasa utawala wa kisheria ni mkubwa sana haina maana kwamba marais wengine hawajafanya wamefanya sana,”alisema Wakili Mavare.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, akizungumza kwenye uzinduzi wa Kigoda cha Utafiti cha Mkapa.

Aliyekuwa Mzungumzaji Mkuu kwenye uzinduzi wa Kigodo cha Utafiti cha Mkapa,  Balozi Ombeni Sefue, alimuelezea Hayati Mkapa alikuwa  mcha Mungu, aliheshimu uhuru wa imani ya kuabudu ya kila mtu, siku zote alisisitiza kwamba masuala ya imani lazima yawe mambo ya  mtu binafsi yasiwe na nafasi katika uongozi wa nchi.

kwa hili alikuwa mfano bora imani yake haikuingilia maamuzi yake kwa namna ya kufanya upendeleo mwaka 1998 alifanya uamuzi wa kuwarejeshea makanisa baadhi ya shule zilizokuwa zimetaifishwa na serikali waanzishe vyuo vikuu vya kusomesha watanzania wa dini zote, alichukua chuo cha serikali akawapa waislamu waanzishe chuo hakuwa na ubaguzi,”alieleza Balozi Sefue.

Alisema Hayati Mkapa lipenda sana kusoma vitabu na majarida mbalimbali maana aliami vitabu ni muhimu katika kurutubisha akili, nafsi na  moyo, aliamini utamaduni wa kusoma vitabu ni sehemu muhimu ya kujenga uwezo wa uongozi.

“Alianzisha mpango wa kuimarisha mazingira ya biashara Tanzania ambayo haikuwalenga wawekezaji wakubwa ilikuwa kwa ajili ya wawekezaji wadogo wa ndani ya nchi kutambua vipato vyao vya kukuza biashara zao, alianzisha TASAF, ili kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini waweze kujikwamua kiuchumi bila kujenga utegemezi kwa serikali, alianzisha MKURABITA kwa kweli Hayati Mkapa alifanya mambo mengi sana kwa faida ya watanzania nikisema niyataje yote itanichukua siku nzima,”alisema Balozi Sefue.

Sehemu ya washiriki waliohudhuria.

Mjane wa Hayati Mkapa, Anna Mkapa, alimuelezea marehemu mume wake  kwamba alikuwa ni baba bora wa familia na taifa kwa ujumla kwani alipenda watu wake waishi kwa amani  pia alipenda kufanya maamuzi yenye kuleta tija na manufaa kwa taifa na kila alipopata nafasi aliutumia muda huo kusali.

Hayati Mkapa alizaliwa Novemba 12, 1938, alifariki Julai 24, 2020, uzinduzi  huo ulifanyika ikiwa ni siku ya kumbukizi yake ya kuzaliwa pia kitabu chake kilichotafsiriwa kwa lugha ya kiswahili alichokiandika kwa lugha ya kiingereza  enzi za uhai wake kiitwacho Maisha yangu, kusudi langu kilizinduliwa huku watu wa kada mbalimbali wakishuhudia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles