JEDDAH, SAUDI ARABIA
WATOTO wa mwandishi aliyeuawa Jamal Khashoggi wamepatiwa majumba ya thamani ya mamilioni ya dola na kulipwa maelfu ya dola kila mwezi na Serikali ya Saudi Arabia, imedaiwa.
Watoto wake wanne, wawili wa kiume na waliobakia wa kike kila mmoja amepewa nyumba zenye thamani ya dola milioni nne sawa na zaidi Sh bilioni tisa kila moja, imeripotiwa.
Pia wanapatiwa dola 10,000 sawa na Sh milioni 23 kwa mwezi pamoja na nyongeza nyingine ya makumi kwa mamilioni ya dola zitakazotolewa mara kesi dhidi ya wanaotuhumiwa kumuua Khashoggi itakapokamilika.
Malipo hayo yanadaiwa kulenga kuhakikisha watoto hao wanabakia kimya kutotoa matamko dhidi ya utawala wa Kifalme,’ Gazeti la Washington Post la Marekani limeripoti.
Gazeti hilo lilizungumza na maofisa wa Saudia wanaohusika na makubaliano hayo.
Nyumba walizopatiwa ziko katika eneo moja lenye uzio mkubwa mjini hapa, huku ile kubwa akipatiwa mwanae mkubwa Salah, ambaye ni mtoto pekee anayeishi moja kwa moja Saudi.
Watoto watatu wengine, mabinti Noha na Razan, na mwana Abdullah, wanaishi Marekani na hivyo wanatarajia kuziuza mali hizo kwa vile hawana mpango wa kuishi hapa.
Lakini Saudi Arabia imekana kuwa malipo hayo ni ‘fedha za damu’ zinazolenga kuiziba mdomo familia hiyo, ikidai ni sehemu ya utamaduni wa Kiarabu.
Serikali Ilikumbushia namna taifa hili lilivyo na utamaduni wa kutoa msaada wa fedha kwa waathirika wa machafuko ya jinai.
Khashoggi, mwanasafu wa gazeti la Washington Post na mkosoaji mkubwa wa familia ya kifalme ya Saudia aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa taifa hili mjini Istanbul, Uturuki Oktoba mwaka jana.
Mwana Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman amekuwa akituhumiwa kuamuru mauaji hayo, lakini ufalme umekuwa ukimtetea kuwa hakuhusika licha ya kuwapo ushahidi.