SAUDI ARABIA, Falme za Kiarabu
SERIKALI ya Saudi Arabia imesema kwamba haitamruhusu mtu yeyote kupata fedha za ugaidi na kueneza chuki na kwamba itashirikiana na Serikali ya Urusi ili kupambana na vitendo hivyo.
Hayo yalisema juzi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akiwa ziarani nchini Urusi.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kueneza chuki, kutoa fedha za aina ya itikadi hiyo au ugaidi,” alisema waziri huyo.
“Nia yetu ya kukabiliana na vitendo hivyo ni ya dhati, tumewaondoa maelfu ya maimamu kwenye misikiti kutokana na uharibifu, tunasimamia mfumo wetu wa elimu ili kuondokana na uwezekano wa kutafsiri maandiko vibaya,” aliongeza waziri huyo.
Alisema ili kutimiza mpango huo, Serikali ya Riyadh itakuwa ikishirikiana na ya Moscow katika kupigana na ugaidi.