29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Samia ataja wabunge wa CCM watakaokatwa Uchaguzi Mkuu

Na GUSTAPHU HAULE

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema mwaka huu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitawang’oa wabunge mizigo.

Alisema watakaopitishwa ni wale ambao wamepimwa kulingana na kazi walizofanya wakiwa madarakani na kwamba mbunge ambaye hakufanya kitu jina lake litakatwa.

Mbali na hilo, alisema wengine watakaokatwa ni wale walioanza kujipitisha mapema majimboni kwa kutoa fedha, ambao majina yao yapo.

Samia alitoa kauli hiyo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa kwa CCM kwa Mkoa wa Pwani  yaliyofanyika viwanja vya Sabasaba, Picha ya Ndege, Kibaha.

Alisema mwaka huu ni wa uchaguzi, hivyo yapo majungu, chuki na misuguano baina ya viongozi wa chama, wabunge na Serikali, kwahiyo lazima watu wajipime mapema.

Alisema kwa sasa tayari watu wameanza kujipitisha kusaka ubunge wakati muda bado na wanachokifanya wanavizia wenzao wapo bungeni halafu wao huku nyuma wanafanya fujo na kwamba chama hakiwezi kuvumilia mambo hayo.

“Wale wote wanaojipitisha mapema watakuwa wamechangia chama maana wanavunja utaratibu kwa kuwa muda wa uchaguzi bado.

“Na kama mtu anataka kugombea, ni vizuri akasubiri muda ufike ili kuwapisha wabunge waliopo madarakani wafanye kazi zao bila usumbufu,” alisema Samia.

Alizitaka kamati za siasa kuacha fitina, chuki na majungu na wafanye kazi bila kuogopa mgombea na kama wataona mtu alijipitisha mapema wamkate jina bila kuogopa na kwamba kufanya hivyo itasaidia chama kupata viongozi waadilifu.

Hata hivyo, katika hatua nyingine Samia aliongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa Pwani kwa kuchangia Sh milioni tano.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno, alisema mtaji wa CCM ni wanachama na kwamba wapo tayari kukisimamia chama wakati wote.

Maneno alisema mwaka huu Serikali inaelekea katika uchaguzi mkuu, hivyo chama kitahakikisha kinampigania Rais Dk. John Magufuli ili aweze kushinda kwa kishindo, lengo likiwa kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo zaidi.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka (CCM) alisema jimbo lao lipo imara katika utekelezaji wa ilani na chama kinaendelea kushirikiana vizuri ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa.

Koka alisema Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu ya barabara, ukiwemo mradi mkubwa wa njia nane ambao unaishia mizani ya zamani.

 Alitumia nafasi hiyo kumwomba Makamu wa Rais kuwa barabara hiyo ya njia nane ifike Kibaha kwa Mathias.

Alisema barabara hiyo ikiishia hapo itavuruga Mji wa Kibaha kwa kutengeneza foleni ya magari, lakini ikivuka na kufika kwa Mathias itasaidia kupendezesha mji na hivyo kusaidia wananchi kiuchumi.

Mbali na hilo, pia alishukuru ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibaha na kusema majengo yote yamekamilika, lakini aliiomba vifaa tiba vipelekwe mapema ili kuwasaidia wananchi kupata huduma kama ilivyopangwa.

Kuhusu wananchi waliopitiwa na mradi wa umeme wa KVA 400 kutoka Kinyerezi hadi Arusha, Koka alisema tathmini imefanyika miaka mitano iliyopita, lakini hadi sasa hawajalipwa fidia zao, hivyo ameomba Serikali iwalipe mapema ili waweze kutumia fedha hizo kwa kufanyia maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alisema mkoa umetekeleza ilani kwa asilimia 90 na kwamba ifikapo Oktoba yale yote yaliyoahidiwa yatakuwa yametekelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles