Na Mwandishi Wetu-ZANZIBAR
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi wa Tanzania Zanzibar waache tabia ya kuwaoza wasichana wa kike wakiwa na umri wadogo bali wawasomeshe kwa ajili ya manufaa yao ya jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo aliitoa juzi kwa nyakati tofauti wakati akizindua madrasa ya kisasa iliyojengwa kwenye eneo la kilimani na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote nchini Tanzania unaojengwa katika eneo la Ijitimai kidoti katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa michango ya wananchi katika siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Kisiwani Unguja.
Alisema kama wazazi na walezi watasomesha watoto wa kike elimu watakayopata itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana hao kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika jamii.
“Elimu kuwa ni haki ya msingi kwa mtoto wa kike hivyo ni muhimu kwa jamii nzima ya Zanzibar ihakikishe watoto wa kike wote wanapata elimu kwani watakuwa na uwezo wa kuchagua na kuandaa mustakbali wa maisha yao ya baadaye ikilinganishwa na hali ilivyo sasa kwenye baadhi ya maeneo,” alisema Samia.
Kuhusu elimu ya dini, Samia aliwahimiza wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema kwa kuzingatia maandiko matakatifu ya Mtume Muhammad (S.A.W).
Alisema vijana wengi wanaolelewa kwa kufuata misingi bora ya dini ni vigumu kurubuniwa na kujiingiza katika matendo yasiyofaa katika jamii.