MWANDISHI WETU –UBELGIJI
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, ameiongoza timu yake ya KRC Genk kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya wenyeji, Sint-Truiden, katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji uliochezwa Uwanja wa Sint-Truiden, St. Trond.
Kwa ushindi huo, Genk ambayo huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza kwa mwaka 2019,
ilifikisha pointi 51, baada ya kucheza mechi 22 na kuendelea kuongoza ligi hiyo
kwa tofauti ya pointi 10 na Club Brugge iliyoko nafasi ya pili.
Katika mchezo huo, Samatta, alifunga bao moja, huku akitengeneza jingine.
Samatta alifunga bao
lake dakika ya 29, akimalizia pasi ya mshambuliaji, Dieumerci N’Dongala, raia
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Bao hilo lilikuwa la kusawazisha baada ya Jordanaa Botaka ambaye pia nia raia wa DRC kuifungia Sint-Truiden bao la kuongoza dakika ya pili ya mchezo huo.
Mfaransa, Yohan Boli,
aliifungia Truiden bao la pili dakika ya 70 kabla ya Samatta kumpa pande safi
mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard, ambaye aliifungia bao la kusawazisha
Genk dakika ya 75.
Genk ilipata nguvu zaidi baada ya kusawazisha na kufanikiwa kuandika bao la ushindi dakika ya 80 kupitia kwa Mkongomani, N’Dongala, aliyemalizia pasi ya Trossard.
Samatta alipumzishwa dakika ya 90 na nafasi yake kuchukuliwa na Zinho Gano.
Samatta mwenye umri wa
miaka 26, amefikisha mabao 55 katika mechi 138 za mashindano yote alizoichezea
KRC Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya DRC.
Kwenye Ligi ya Ubelgiji ametupia mabao 40 katika
mechi 106, wakati Europa League amefunga mabao 14, katika mechi 22 na katika
Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa