Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
TUKIO la kutoweka kwa msanii wa Bongo Fleva anayeimba mtindo wa hip hop nchini, Ibrahim Mussa maarufu Roma Mkatoliki, limeendelea kuzua sintofahamu baada ya jana Jeshi la Polisi kukana kumshikilia.
Kutokana na hilo, wasanii wameiomba Serikali kuingilia kati kwa kufanya uchunguzi wa kina kupitia vyombo vyake vya usalama.
Roma akiwa na wasanii wenzake wanadaiwa kutekwa juzi Alhamisi na watu wasiojulikana wakiwa kwenye Studio za Tongwe Records, Masaki jijini Dar es Salaam, walipokuwa wakifanya shughuli zao za kawaida.
Mbali na Roma wengine wanaodaiwa kutekwa ni pamoja na msanii Moni Centrozone, Bin Laden na Imma ambaye ni mfanyakazi wa mama mzazi wa mmiliki wa studio hizo, Junior Makame.
Jana baadhi ya wasanii waliitisha mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa ufukwe wa bahari wa Coco na kueleza juhudi ambazo wamezifanya za kuwasaka akina Roma pasipo mafanikio.
Akizungumza katika mkutano huo, Junior alisema hadi sasa bado haijajulikana wasanii hao walipo pamoja na jitihada za kuripoti na kukagua katika vituo vya polisi.
“Tunaomba Serikali itusaidie na wananchi huu si wakati wa kulalamika na kushutumu mamlaka zozote kwakuwa hakuna anayejua wasanii hawa walipo,” alisema Junior.
Katika mkutano huo ambao ulijumuisha wasanii mbalimbali nchini, Junior alisema lengo la mkutano huo si kumlaumu mtu wala vyombo vya Serikali isipokuwa ni kuomba ushirikiano kwa jamii.
Akielezea tukio hilo, Junior alisema siku hiyo alishinda studio na ilipofika muda wa jioni Roma alimpigia simu na kumwambia kuwa anakuja kurekodi.
Alisema baada ya simu ya Roma, alipigiwa simu kutoka nyumbani kwake akielezwa kuwa mtoto wake anaumwa na anatakiwa kufikishwa hospitali hivyo alilazimika kuondoka.
“Nimetoka nimefika tu nyumbani baada ya muda kuna dada alinipigia simu ambaye na yeye kwa muda huo ndio alikuwa anaingia studio na kunieleza kuwa kuna watu wamekuja wakiwa kwenye gari aina ya Noah walimhoji Roma baadaye waliwahoji watu wengine kisha wakaingia studio na kuchukua televisheni pamoja na kompyuta,” alisema Junior.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo alilazimika kurudi tena studio kabla ya baadaye kuanza kufanya mawasiliano na watu mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.
“Baada ya kupata taarifa hiyo kwa undani nilimpigia simu kaka yangu Ruge nikamwelezea yaliyotokea studio, akanishauri niende kutoa taarifa polisi nikaenda Oysterbay polisi, nikaripoti lakini sikupaswa kutoa maelezo kwa sababu sikushuhudia tukio na kulazimika kuchukua maelezo kwa mtu ambaye alinipigia simu, baada ya kuchukua maelezo hayo walifungua shauri lenye RB namba 0B/RB/72/017,” alisema Junior.
Alisema shughuli za kuchukua maelezo kituoni hapo ambapo alikuwa ameambatana na Ruge, ziliwafanya kukaa eneo hilo hadi saa saba usiku na baadaye alilazimika kumpigia simu mke wa Roma, Nancy akimtaka kuwa na subira kwa kuwa suala la mume wake linashughulikiwa.
“Vitu walivyochukua sivifikirii sana, nawafikiria wasanii wangu wapo wapi, mali nitanunua lakini siwezi kununua roho za wasanii waliochukuliwa,” alisema Junior.
Alisema ingawa simu za viganjani za wasanii hao bado zipo hewani lakini hazipokelewi jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa na hofu.
Akizungumzia tukio hilo huku akibubujikwa na machozi, mke wa Roma aitwaye Nancy aliomba ushirikiano na wananchi katika kipindi kigumu alichonacho.
“Sina mengi, kikubwa naomba ushirikiano wenu, naomba msaada kutoka vyombo vya sheria na polisi,” alisema Nancy huku akilia na kuondoka katika eneo alilowekewa vipaza sauti.
Naye Katibu wa Shirikisho la Muziki wa Kizazi Kipya (Tuma), Samweli Mbwana maarufu Briton alisema: “Tumeongea na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na ameshaunda kikosi maalumu kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.
“Katika kuonyesha msisitizo, Kamishna Sirro ametuahidi kuonana naye kesho (leo), mkutano ambao utawashirikisha waandishi na wasanii hapo ndipo tutajua wamefikia wapi, kama amewapata ama taarifa yoyote inayowahusu wao,” alisema.
Alisema Kamishna Sirro aliwasisitizia kuacha kutupa lawama kwa Serikali mitandaoni.
Alisema wasanii wanaendelea kusisitiza jamii kuhakikisha wanatoa taarifa kwa yeyote atakayezipata kupitia vyombo husika.
Alisema kwa sasa hawailaumu Serikali isipokuwa wanataka msanii huyo apatikane na kama atakuwa na hatia taratibu za kisheria zifuatwe.
Kutokana na tukio hilo alisema kwa sasa wasanii na wadau wa muziki wameanzisha ‘hash tag’ inayosema ‘Akina Roma wako wapi?’ Lengo likiwa ni kuhamasisha harakati za kuwatafuta wasanii hao.
Baada ya mkutano huo, gazeti hili lilienda moja kwa moja sehemu ilipo studio hiyo ambapo baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walisema wakati mkutano ukiendelea kuna baadhi ya polisi walifika katika eneo hilo wakiwa na magari mawili ya polisi kuuliza kama kuna kitu chochote kinaendelea ndani ya studio hizo.
“Walikuja askari hapa wakiwa na magari mawili, wamegonga wameuliza mkutano wa wasanii kama unafanyika humu tukawaambia hawapo wakaondoka,” alisema mmoja wa wanafamilia hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Kwa upande wa Kamishna Sirro, alisema wameshafungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio hilo na wanaendelea kufuatilia.
“Mambo haya yana mambo mengi sana, inawezekana ni watu wabaya wamefanya hivyo, tuangalie je, kuna mambo ya ugoni au ugomvi mwingine, kupitia watu wetu wa Cyber. Wananchi wasihukumu, kunapotokea jambo kila kitu kinaongelewa lakini wasiihusishe Serikali,” alisema Kamishna Sirro.
Alisema atatoa taarifa kamili leo saa 5 asubuhi kwa kufanya mkutano na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa watu waache kuvumisha mambo na kusingizia Serikali bila kutaja mhusika.
Baadhi ya wasanii waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Chege, Mwasiti, Madee, Babu Tale na Navy Kenzo.