Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM
NI unyama usio na kifani. Ndivyo unavyoweza kusema mara baada ya kumwona na kusikiliza maswahibu yaliyomkuta kijana Said Michael (28) mkazi wa Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam. Kijana huyu alifanyiwa unyama wa kutisha na watu wasiojulikana.
Wiki iliyopita, Said kwa msaada wa msamaria mwema alifika katika Ofisi za Kampuni ya New Habari (2006)Ltd zilizopo maeneo ya Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam ili kuelezea masahibu yaliyomkuta Agosti 5, 2015 baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kumfanyia unyama uliomsababishia maumivu makali hadi hivi sasa.
Akisimulia historia yake, anasema yeye ni mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza maeneo ya Pasiasi, ukoo wao ni waumini wa dini Kikristo lakini alitengena na familia yake baada ya kubadili dini na kuingia kwenye Uislamu.
Anasema kitendo cha yeye kubadili dini kiliwaudhi ndugu zake na hivyo kujikuta katika migogoro ya hapa na pale.
Anasema kuwa jambo hilo lilikuwa likimkosesha amani hivyo akaamua kuja jijini Dar es Salaam kuanza maisha upya. “Wazazi na ndugu walinitenga na hata mke wangu tuliachana kutokana na uamuzi wangu wa kubadili dini. Nilipofika hapa mjini niliendelea na masomo ya dini huku nikijishugulisha na shuguli za ulinzi katika Sheli ya Muza Oil, kazi niliyoifanya kwa muda wa miezi mine,” anasema Michael.
Akizungumzia ukatili aliofanyiwa na watu wasiojulikana, anasema kamwe hawezi kuisahau siku hiyo kwa kuwa ilichangia kuharibu maisha yake kwa kiasi kikubwa.
Anasema ilikuwa ni majira ya usiku wa Agosti 5 mwaka 2015 ambapo akiwa nyumbani kwake walifika watu wakagonga mlango, alipowahoji kuwa ni kina nani mmoja wao akajitambulisha kwa jina moja la Alfan, jina ambalo ni la mwajiri wake wa zamani.
“Niliposikia kuwa ni Alfan nikawafungulia, cha ajabu walipoigia ndani nikakuta watu tufauti na walivyojitambulisha, wakanikamata na kunifunga kitambaa na kunipeleka kusikojulikana.
“Kwakweli walinitesa mno, nilikuwa katika mateso kwa muda wa takribani wiki nzima, nilipigwa na nondo, walipoona haitoshi wakanipiga risasi katika mguu wa kulia ukavunjika. Baada ya hapo wakanichoma kwa ujiuji wa dumu la plastiki lililochomwa na moto,” anasema Michael.
Anasema wakati akiendelea kupatiwa mateso, jambo walilokuwa wakimuuliza ni kwanini aliamua kubadilisha dini na kutengena na familia yake.
“Walipekuwa kwenye simu yangu wakakuta namba ya Ostadh Ramadhani ambaye ni mwalimu wa Madrasa Geita, wakaanza kusema eti wanamuhitaji yeye.
“Katika kipindi cha wiki nzima nilikuwa nahojiwa na watu wanane kabla yule ambaye aliwatuma hajafika. Mhusika alikuja siku ya saba hapo ndipo mateso yaliongezeka maradufu kwani ilifika wakati nikapoteza fahamu nikajitambua nikiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,” anasimulia kwa uchungu.
Michael anasema kuwa katika maisha yake hakuwahi kugombana na mtu yeyote yule, hivyo anawashangaa watu ambao waliamua kumfanyia ubaya huo.
“Katika makuzi yangu sikuwahi kukwazana na mtu yeyote zaidi ya familia yangu ambapo chanzo kilikuwa ni kubadili dini, hivyo nilijikuta nikihisi kuwa huenda familia yangu imeamua kuniangamiza kutokana na misimamo yangu ya kidini,” anasema.
Anasema kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibu alifikishwa hospitali na wasamaria wema baada ya kumuokota porini akiwa na hali mbaya.
“Madaktari walisema hali yangu ilikuwa mbaya mno, kwani licha ya mateso ya hapa na pale waliyonipa, hawakutaka kuniacha hivi hivi wakaniingiza mti kwenye sehemu ya haja kubwa hivyo kunisababishia kutokwa na damu nyingi pia haja kubwa kutoka yenyewe bila taarifa.
“Namshukuru Mungu Muhimbili nilipatiwa matibabu lakini kutokana na hali niliyokuwa nayo iliwalazimu wanipe rufaa nikatibiwe nchini India. Nilikaa India kwa miezi mitatu na nilipopata nafuu nilirudi nchini lakini hali haikuwa nzuri kwani bado damu iliendelea kutoka kidogo kidogo,” anasema na kuongeza:
“Niliporudi nchini niliendelea kwenda Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya kawaida lakini hali ilivyozidi kuwa mbaya nilitakiwa kurudi India kwa mara ya pili kwa matibabu zaidi. Sikuwa na kitu chochote wala fedha ya kuniwezesha kufika India hivyo nililazimika kuchangisha kwenye miskiti na taasisi mbalimbali hadi nikafanikiwa kwenda na kutibiwa.”
Anasema kuwa licha ya matibabu yote aliyokuwa akiyapata awali, hali yake bado inaendelea kuwa mbaya kwani sasa hivi hadi kutembea kwake ni shida, hivyo anapaswa kurudi kwa mara nyingine hospitalini lakini inashindikana kutokana na ukosefu wa fedha.
“Licha ya hali niliyonayo kama unavyoniona, nimekuwa nikizunguka kwa watu, mashirika na taasisi mbalimbali kuomba msaada wa kifedha ili ziniwezeshe kwenda kupatiwa matibabu lakini bado sijafanikiwa.
“Kuna msamaria mwema aliona taarifa zangu kwenye vyombo vya habari akanisaidia Sh 200,000 lakini nimejikuta ikiishia kwenye matumizi ya kawaida bila lengo kutimia,” anasema.
Anasema kuwa kwa sasa anahitaji Sh milioni tatu ili aweza kwenda India kupata matibabu lakini tangu niambiwe kuwa inabidi niende huko ni kipindi kirefu kimepita.
“Nawaomba Watanzania wanaisaidie kiasi hicho cha fedha ili niwahi matibabu, kwani niliwekewa mpira sehemu ya njia ya haja kubwa ambao umekaa muda mrefu bila kutolewa hivyo tayari umeoza na unamsababishia kutokwa na damu, kukaa chini pia nashindwa. Naishi katikawakati mgumu mno,” anasema Michael na kuongeza kuwa mpira huo hauwezi kubadilishwa na daktari yeyote yule hapa nchini zaidi ya India walikomwekea.
Akiwazungumzia mkewe na watoto wake, anasema kuwa mkewe alimtelekeza baada ya kubadili dini, akawa anaishi na watoto wake ambao baada ya kupata matatizo aliamua kuwasafirisha kwenda Mwanza.
“Mke wangu naye hakukubaliana na uamuzi wangu hivyo, aliamua kuondoka na kurudi kwao na tangu siku hiyo hatukuwahi kuwasiliana. Watoto nilikuwa naishi nao lakini baada ya kupata matatizo haya na kukosa namna ya kuwatunza nikiwa katika hali hii niliamua kuwasafirisha kurudi Mwanza,” anasema.
Anasema kuwa amejaribu mara kadhaa kuwatafuta ndugu zake kwa njia ya simu lakini akipiga wakisikia sauti yake wanakata.
Kutokana na hali hiyo anawaomba wasamaria wema wamsaidie kiasi chochote cha fedha walichonacho kupitia namba 0742355183.