MONROVIA, LIBERIA
UNAPOLITAJA jina la George Weah, ni jina kubwa na lenye maana Afrika hususani mashabiki wa kandanda.
Hadi makala haya yanapoandikwa kutoka katika ardhi yenye nchi 54 George Weah ndiye aliyetwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ulaya, Afrika na Dunia katika msimu mmoja mwaka 1995.
Weah aliwahi kuzichezea klabu za soka za Monaco, PSG, AC Milan, Chelsea na Manchester City.
Makala haya yanaangazia safari yake ya maisha ya kawaida katika soka na siasa. Hivi sasa George Weah anawania kiti cha urais nchini Liberia.
Oktoba 10, mwaka huu wananchi wa Liberia walifanya Uchaguzi Mkuu nchini humo wa kumchagua Rais wa Taifa hilo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa George Weah anaongoza dhidi ya mpinzani wake wa karibu sana ambaye ni makamu wa Rais wa taifa hilo, Joseph Boakai.
Licha ya dosari za hapa na pale Tume ya Uchaguzi nchini humo inatarajiwa kumtangaza mrithi wa Rais Ellen Johnson Sirleaf muda wowote huku maelfu ya wananchi wakiwa na matamanio kumwona staa huyo wa soka George Oppong Weah akitangazwa mshindi.
Ellen Sirleaf ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika ambaye alishinda uchaguzi wa 2005 kufuatia kipindi cha mpito baada ya vita na baadaye alitetea tena nafasi yake 2011.
Watu milioni 2.1 walioandikishwa walipiga kura zao kumchagua rais kutoka idadi ya wagombea 20, ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja na kuwachagua wabunge 73 wa baraza la wawakilishi.
Iwapo kati ya wagombea hao hakuna atakayefikisha asilimia 50 wagombea wawili waliopata idadi kubwa watachuana tena kwenye duru ya pili itafanyika Novemba 7. Wachambuzi wa mambo wameashiria uwezekano wa uchaguzi huo kwenda duru ya pili.
MBIO ZA URAIS
Baada ya kumalizika kwa vita vya pili vya ndani ya Liberia, George Weah akawania urais katika uchaguzi wa mwaka 2005 kupitia chama cha Congress for Democratic Change (CDC).
Pamoja na kuwa maarufu zaidi nchini Liberia, upinzani ulitumia kampeni zake kumkosoa kwa kukosa elimu ya darasani kama kikwazo cha yeye kuiongoza nchi ukilinganisha na mpinzani wake, Ellen Johnson Sirleaf ambaye alisoma katika Chuo Kikuu cha Harvard.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Liberia walimzungumzia, Weah kama mwanasiasa asiye na uzoefu, Ellen aliwahi kuwa waziri wa fedha kuanzia miaka ya 1970 huku akifanya kazi katika benki ya dunia.
Aidha, katika kinyang’anyiro hicho cha urais Weah aliwekewa pingamizi kutokana na awali kupewa uraia wa Ufaransa akiwa klabu ya Paris Saint Germain (PSG) aliyoichezea tangu mwaka 1992 hadi 1995. Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali pingamizi dhidi yake.
Katika uchaguzi huo Weah alitikisa nchi nzima kutokana na umaarufu wake hata hivyo matokeo ya mwisho ya uchaguzi yalimpa ushindi mwanamama Ellen Sirleaf aliyepata asilimia 59.4 dhidi ya asilimia 40.6 alizopata George Weah.
Matokeo hayo ya uchaguzi yalisababisha vurugu kutoka kwa wafuasi wa Weah ambao hawakuridhishwa na taratibu za uchaguzi pamoja na matokeo. Baadaye wafuasi hao waliombwa kukubali matokeo kwani uchaguzi ulikuwa halali.
Suala la elimu lilikuwa tata nchini Liberia kutoka kwa wapinzani wake hata kumfanya ashindwe kugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2011 dhidi ya Ellen Sirleaf.
ALIKOTOKA
Mwanasiasa huyo alizaliwa Oktoba 1, 1966 huko Grand Kru, Liberia. Alitangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1995, huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara tatu. Mwaka 2004 aliandikwa katika orodha ya wachezaji 100 bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambao bado wanaishi.
George Weah alitua barani Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kusajiliwa na kocha Arsene Wenger wakati akiifundisha AS Monaco ya Ufaransa. “Weah ana kipaji cha ajabu. Sijawahi kuona mchezaji akijituma uwanjani kama yeye,” alikaririwa kocha wa sasa wa Arsenal, Arsene Wenger
Mwaka 1991 Weah alikuwa katika kikosi cha Monaco kilichotwaa Kombe la Ligi ya Ufaransa. Kati ya mwaka 1992 hadi 1995 aliichezea Paris Saint Germain na kutwaa makombe mbalimbali kisha kuibuka mfungaji bora wa klabu bingwa Ulaya msimu wa 1994-1995.
Weah alijiunga na AC Milan msimu wa 1995-1996 na kushinda kikombe cha Ligi ya Italia 1996 na 1999. Mwaka 1995 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia. Weah alikuwa mchezaji maarufu zaidi katika kikosi cha AC Milan kutokana na uwezo pamoja na mabao maridadi.
Baada ya kuondoka Milan Januari 2000, Weah alijiunga Chelsea na baadaye Manchester City na Olympique Marseille kwa mafanikio ya haraka, kabla ya kuondoka Marseille mwezi Mei 2001 akielekea Al Jazira FC ya Falme za Kiarabu, ambako alicheza na kustaafu soka lake mwaka 2003.
MISAADA NA LIBERIA
Pamoja na mafanikio makubwa katika ngazi ya klabu, Weah alishindwa kufanya hayo akiwa na timu ya Taifa ya Liberia. Alifanya kila alichoweza katika timu ya taifa katika kucheza, kufundisha na kuiwezesha kifedha lakini akishindwa kuisaidia kufuzu hata mara moja katika fainali za kombe la dunia.
Weah aliichezea Liberia michezo 60 katika kipindi cha miaka 20 na kufunga magoli 22. Amekuwa ni mchezaji muhimu wa Liberia huku akiwa kocha kipindi fulani na kuwawezesha kifedha.
FAMILIA
Weah ni baba wa watoto wanne aliozaa na mkewe mwenye asili ya Jamaica, Clar. Watoto wao ni George Jr, Martha, Timothy George na Jessica.
Hadi sasa macho na masikio ya mashabiki wa soka yanasubiri kuona na kusikia matokeo ya urais yakitangaza, ushindi wa George Weah.