NA ELIYA MBONEA, ARUSHA
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Khamis Juma amesema, ndani ya vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) hakuna jina la mgombea litakalokatwa bila kumuonea mtu.
Kauli hiyo aliitoa juzi jijini hapa katika sherehe za kumwapisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wa Wilaya ya Arusha DC, Mathias Manga kuwa Kamanda wa vijana wa wilaya hiyo.
Akizungumza na mamia ya wanachama na viongozi wa CCM kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha Sadifa alisema, wakati huu wa sasa si wa kukata majina ya wagombe ovyo ovyo.
“Nimesikia maneno eti wanangoja majina mengine yakatwe kwenye CC, nawaambieni hakuna jina litalokatwa kijingajinga hizi si enzi za kukatana majina,” alisema Sadifa na kuongeza.
“Kwanza hao wanaosema hayo maneno wao si wajumbe wa vikao hivyo. Na Rais Jakaya Kikwete alisema kwenye kikao hatakatwa mtu kijinga kama anakubalika kwa watu kwanini akatwe.
“Chagueni mtu wenu kwa umakini, nawaomba msitishwe hizo ni propaganda. Wajumbe wa CC ndio sisi hakuna mtu atakayekatwa jina kijinga,” alisema.
Sadifa alitumia fursa hiyo pia kuwaeleza wana CCM hao kutoka mikoa mitatu kuwa UVCCM hakijawahi kutuma kiongozi wake kwenda kutukana watu wala viongozi.
“Siasa za kuchafuana sizipendi na ukiona mtu wa CCM anapanda jukwaani kuchafua viongozi huyo ni mjinga na hana maadili. UVCCM wala CCM hatujamtuma mtu kwenda kutukana viongozi wa nchi,” alisema Sadifa.
Akizungumzia kuhusu kuelekea uchaguzi mkuu na hatua za baadhi ya wana CCM kutangaza nia Sadifa alisema, kutangaza nia si kosa wala dhambi.
Alisema pamoja na wanachama wengi kuendelea kutangaza nia wakitaka wateuliwe bado kwa mahali taifa lilipofikia linahitaji kuwa na rais mwenye sifa za kujiamini na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi magumu.
“Tanzania ya leo si ile ya akina Mwalimu Nyerere, leo tunahitaji kuwa na rais mwenye sifa za kujiamini na uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa faida ya nchi,” alisema Sadifa.
Kwa upande wake Mjumbe wa NEC na Kamanda wa Vijana wa Arusha DC iliyopo Jimbo la Arumeru Magharibi Manga aliwaomba wana CCM kuungana na kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Nawaomba tukae pamoja, tukifanikiwa kupata mgombea kutoka Kanda ya Kaskazini tushirikiane kwa kuwa kitu kimoja. Tuondoe tofauti zetu tuwe watoto wa familia moja,” alisema Manga.