ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kumwondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Rasilimali (TIB), Frank Nyabundege, sababu za uamuzi huo zimebainika, ikiwamo ufanisi usioridhisha wa benki hiyo.
Taarifa iliyotolewa na BoT kupitia Idara ya Uhusiano wa Umma na Protokali, ilieleza juzi kuwa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 33 (1) na 33 (2) (f) ya Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006, BoT imeamua kusimamisha uteuzi wa Nyabundege kama Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, kuanzia Julai 13, mwaka huu.
Uamuzi huu umechukuliwa baada ya utendaji usiofaa wa benki.
Kifungu cha 33 – (1) cha sheria hiyo kinaeleza bayana kuwa: “Benki inaweza kutoa maelekezo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya benki yoyote au taasisi ya kifedha, maelekezo ya tabia ya jumla au maalum kuhusu utendaji wa kazi na kuhusiana na masuala yanayoonekana kuathiri shughuli za benki kwa masilahi ya taifa, na bodi itatekeleza kwa vitendo maagizo hayo.”
Hata hivyo kinasindikiziwa na kifungu cha 33 (2)(f) ambacho kinaainisha kuwa baada ya utekelezaji wa kifungu cha awali cha 33(1), BoT inatakiwa: “Kuanzisha utaratibu wa kisheria wa kuondolewa, au kutoa amri ya kusimamishwa inayohitaji mkurugenzi au ofisa yeyote au mtu mwingine au watu katika nafasi ya usimamizi wa benki au taasisi ya kifedha, kuacha kushiriki katika mambo ya benki au taasisi ya kifedha kwa muda mfupi au wa kudumu.”
Taarifa hiyo ya BoT ilieleza; “Kwa hiyo, kwa mujibu wa majukumu ambayo Benki Kuu ya Tanzania, kama ilivyoagizwa chini ya kifungu cha 33 (2) (b) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006 imemteua Fred Luvanda, kutoka Idara ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha kusimamia masuala na shughuli za kila siku za TIB kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji.”
BoT katika taarifa yake ilieleza kuwa uteuzi huo wa Luvanda kama ilivyoainishwa, unatokana na kifungu hicho cha 33(2)(b) kinachoipa mamlaka BoT “kumteua mtu ambaye, kwa maoni ya benki, amepata mafunzo na ujuzi sahihi kushauri benki au taasisi za kifedha juu ya hatua za kuchukuliwa ili kurekebisha hali yake, na kutayarisha mshahara wake ambao utalipwa na benki au taasisi ya kifedha.”
Uteuzi huo ni sehemu ya hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na BoT katika siku za hivi karibuni, ambayo imekuwa mwiba katika kusimamia taasisi za kifedha ambazo zimekuwa hazioneshi ufanisi.
Katika taarifa yake, BoT ilieleza kuwa hatua hii imechukuliwa ili kuboresha uangalizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Benki Kuu ya Tanzania ingependa kuwajulisha umma kuwa TIB itaendelea kutoa huduma zote za kibenki ikiwa ni pamoja na malipo ya majukumu yaliyostahiki.
“Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda masilahi ya wote walioweka fedha zao katika benki hiyo na kudumisha uimara wa sekta ya benki,” ilieleza sehemu ya taarifa yake.
BoT imekuwa ikichukua hatua kwa benki kadhaa nchini, ikiwemo kuzifutia leseni na kuziweka chini ya mufilisi benki za Covenant Bank For Women (Tanzania) Limited, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited, na Meru Community Bank Limited mwanzoni mwa mwaka jana.
Benki nyingine pia zilipewa muda wa miezi sita kukidhi matwaka ya kisheria zikiwemo Benki ya Chama cha Ushirika Kilimanjaro, Benki ya Wanawake (TWB) na Tandahimba Community Bank.
Agosti mwaka jana, BoT pia ilitangaza kuiweka chini ya uangalizi Benki M baada ya kubaini ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.
BoT pia ilitangaza kuridhia muunganiko wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Benki ya Posta na kuwa benki moja itakayoitwa TPB Plc, huku ikiziruhusu Benki ya Wananchi ya Tandahimba (Tacoba) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) kuendelea na biashara baada ya kutimiza masharti ya kuongeza mtaji.
Mwishoni mwa mwaka jana, BoT pia ilianza kuchukua hatua kali dhidi ya maduka ya kubadilisha fedha mkoani Arusha na kuendelea Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo ilieleza kuwa inaandaa kanuni mpya kwa ajili ya kuendesha maduka hayo.