32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU 5  ZA ASLAY KUTUSUA ZAIDI  2017

NA  CHRISTOPHER MSEKENA

MILANGO ya mwanamuziki Aslay imeendelea kufunguka akiwa nje ya bendi ya Yamoto, aliyoifanyia kazi zaidi ya miaka miwili sasa. Kuvunjika kwa bendi hiyo na kila msanii (Maromboso, Enock Bella na Beka Flavour) kuanza kufanya kazi zao binafsi imekuwa ni neema kwa Aslay.

Mfululizo wa kuachia ngoma kila mwezi umempa utambulisho mpya kwa mashabiki ambao walikuwa na kiu ya kumsikia akiwa mwenyewe toka kipindi kile alipotoka kupitia wimbo uliomtambulisha (Nakusemea) na baadaye kuibukia Yamoto Band chini ya kituo cha Mkubwa na Wanawe.

Hivi sasa Aslay ameitawala mitaa kwa ngoma yake mpya inayoitwa Natamba, ambayo ndani ya wiki moja tayari video yake ilikuwa imetazamwa na watu zaidi ya milioni 1.1, huku ikipata nafasi kubwa ya kuchezwa kwenye redio na runinga kutokana na mapendekezo ya mashabiki huku wengine wakimpa nafasi ya kupenya vizuri katikati ya ufalme wa Ali Kiba na Diamond Platnumz.

Juma3tata leo tunakusogezea sababu kubwa tano ambazo zinamfanya Aslay akubalike zaidi kipindi hiki na watu wa rika zote kila anapoachia ngoma mpya.

HAFUNGAMANI  POPOTE

Moja ya vitu ambavyo vinamsaidia Aslay, kufanya vizuri kwenye muziki wake ni kutokuwa na upande wowote, hana timu au kikundi cha watu kwa ajili ya kufanya fitna ili awike, zaidi ya menejimenti na nguvu ya umma (mashabiki) ambayo wameendelea kumsapoti katika kila ngoma anayoitoa.

Tunafahamu timu zinavyoweza kumjenga na wakati huo huo kum bomoa mwanamuziki, hasa pale ambapo timu pinzani inapodhamiria kumwangusha msanii wa upande wa pili. Aslay amekuwa akikwepa kuwagawa mashabiki zake kwa kutokuwa upande wowote ule hasa ule wa mahasimu Ali Kiba na Diamond Platnumz.

TUNGO ZAKE  MUJARABU

Tungo kali za mashahiri kwenye nyimbo za Aslay zimekuwa sababu kubwa ya mwanamuziki huyu kukubalika. Nyimbo kama Angekuona, Pusha, Baby, Likizo, Tete, Usiitie Doa, Muhudumu na Natamba ambazo zote amezitoa mwaka huu kuanzia mwezi Aprili zimesheheni ufundi wa uandishi wa tungo mujarabu zinazotoa elimu na burudani kwa yeyote atakayesikiliza.

Tungo zake zinamgusa mtu yoyote, ameweza kuyaelezea maisha ya watu kupitia nyimbo ndiyo maana kila wimbo anaoutoa unakubalika mtaani.

WANAWAKE NA WATOTO

Soko kubwa la muziki lipo kwa wanawake (wasichana) na watoto, mara nyingi sisi wanamume huwa tunafuata mkumbo tu kutoka kwao. Rejea kwenye wimbo wake wa kwanza, Nakusema, ni wimbo wa kitoto uliopendwa na watoto mpaka watu wazima wakauzimikia.

Hali kadharika katika tungo zake hizi mpya ameendelea kuwaimbia kina dada warembo, ana wabembeleza na wakati mwingine hata kama ujumbe utalenga kumkosoa msichana, atatengeneza mazingira ya kila mwenye jinsia ya kike auelewe na kuupenda hivyo kufanya aendelee kukubalika.

MAISHA YAKE BINAFSI

Aslay ni miongoni mwa wasanii wachache ambao hawapendi maisha yao binafsi yaonekane kwa jamii. Nafahamu mwanamuziki huyu ana mtoto wa kike na mpenzi wake, lakini hajawahi kuwaweka mitandaoni ili kuepuka maisha yake binafsi yasiharibu biashara yake ya muziki.

Hali hiyo inafanya asilimia kubwa ya mashabiki zake wapende muziki wake, wasimfahamu Aslay nje ya muziki kwa skendo za kipuuzi ambazo zimewapoteza wasanii wengi waliowahi kufanya vyema hapo zamani.

UONGOZI IMARA

Aslay ana menejimenti nzuri yenye malengo ya kuhakikisha mwanamuziki huyu anatimiza malengo aliyojiwekea. Yupo kwenye uongozi wa meneja Chambuso ambaye wanafahamina zaidi pamoja na Mx Carter ambaye ni meneja wa biashara wa msanii Shetta.

Msanii ili asimame ni lazima awe na uongozi wenye kiu ya mafanikio, kwa upande wa Aslay amefanikiwa katika hilo kwani Chambuso na Mx Carter ni mameneja wanaofanya kazi yao vizuri ndiyo maana nyimbo zote za Aslay zinaleta mrejesho chanya kwenye biashara yao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles