Amina Omari,Muheza
RUSHWA ya ngono imeelezwa ni miongoni mwa vitendo vya ukatili ambavyo vinaongoza kurudisha nyuma juhudi za maendeleo ya mwanamke nchini.
Hayo yalisemwa na Ofisa Programu Harakati na Ujenzi wa Pamoja kutoka Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai wakati wa semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuripotia habari za jinsia.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2016/18, zinaonyesha asilimia 45 ya wanawake kati ya umri wa miaka 15 -49, wamekuwa waathirika wa ukatili wa kijinsia,huku asilimia 25, ikiwa ukatilia wa kuumizwa mwili.
Alisema vitendo vya unyanyasaji wa kingono,vimekuwapo pale ambapo mwanamke anashida ya kutafuta ajira,fursa za kimasomo na hasa nyakati za uchaguzi
“Vitendo hivi vimekuwa vikichangia kuwaumiza wanawake kisaikolojia na ukandamizwaji wao,”alisema Sangai.
Alisema mtandao huo,umekuwa na kazi ya kusaidia kujengea uwezo wanawake ili kutambua haki zake.
Ofisa Habari wa TGNP, Monica John alisema vyombo vya habari vinajukumu la kuhakikisha wasaidia kundi hilo kupata haki zao .
Alisema kusaidia kundi hilo kutambua haki zao, ikiwamo huduma bora za afya ,ushiriki wa wanawake katika uongozi na chaguzi mbalimbali.
Baadhi wa wanawake wa Kata ya Zirai, walisema mfumo dume wa wanaume kumiliki mali na ardhi, imekuwa ni kikwanzo cha maendeleo ya mwanamke.
“Mwanamke wa vijijini hauna haki ya kushiriki ngazi ya uamuzi,tukiwa sehemu ya wazalishaji tunabaki tunaangalia tu,”alisema Joice Stanley.
Alisema kuwa licha ya kata hiyo kuongoza kilimo cha viungo,ubovu wa barabara umekuwa changamoto ya mazao yao kufika sokoni mapema,” alisema.