Na ZAINAB IDD-DAR ES SALAAM
KATIKA kuhakikisha Tanzania inakuwa na maendeleo katika mchezo wa riadha wa mbio ndefu, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, anatarajia kukutana na waandaaji wa mbio hizo kote nchini Septemba 16, mwaka huu katika Ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam.
Mtaka ameamua kukutana na waandaaji hao ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao mkubwa wanaotoa katika maendeleo ya mchezo wa riadha hapa nchini na jamii kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa RT, Wilhem Gidabuday, ameliambia MTANZANIA kuwa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji kitakachofanyika Septemba 15 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, siku inayofuata waandaaji watakutana na kamati hiyo ili kuangalia mambo gani yanatakiwa kufanyika hivi sasa kwa lengo la kuleta maendeleo katika mbio ndefu.
“Rais RT pamoja na kamati nzima ya utendaji inahitaji maoni ya wadau wa mchezo wa riadha ili kuhakikisha katika miaka minne ya uongozi wake inatimiza malengo ya kupiga hatua mbele katika maendeleo, hivyo haina budi kukutana na waandaaji hao wa mashindano mbalimbali tukianza na wale wa mbio ndefu ili kupata maoni pamoja na mapendekezo kwa masilahi ya riadha Tanzania,” alisema.